Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana ametembelea mabanda ya maonesho katika viwanja vya Nzuguni, Dodoma leo tarehe 04 Agosti 2025, kujionea ubunifu na fursa zinazotolewa na sekta mbalimbali.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mabanda Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewahimiza Watanzania kutumia fursa ya maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane 2025) ili kujifunza mbinu mbalimbali za uzalishaji wa mazao kwa maslahi mapana ya jamii na taifa kwa ujumla.
“Naomba nitoe rai kwa Watanzania tutembelee maeneo haya ya maonesho kuna bidhaa nzuri, kuna utafiti, kuna elimu, kuna mbegu, vivutio vya kila aina na pia unapokuja katika maonesho haya unapata elimu unapata elimu ya aina mbalimbali” amesema Waziri Chana.
Aidha, Waziri Chana ameahidi kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao ili kuongeza mapato kwa taifa na wananchi na pia kuunga mkono Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayoendelea kufanya kazi nzuri kwa watanzania.