Spika wa kwanza wa bunge la kaunti ya Homa Bay Samuel Ochilo amewasuta baadhi ya viongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya wakiongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuhusu kile alichokiita njama zao za kutaka kumpindua Raila Odinga kutoka kwa uongozi wa muungano huo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Citizen TV ya Kenya, Ochilo amemshutumu Kalonzo kwa kupanga kumpindua Odinga baada ya viongozi wanne wa ODM kuteuliwa na Rais William Ruto kwenye baraza lake la mawaziri.
Ochilo amesema mkutano wa wanahabari ulioitishwa na kundi la viongozi wa Azimio kukashifu uteuzi huo, wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, uliashiria mapinduzi dhidi ya uongozi wa Odinga.
Musyoka alifanya mkutano na wanahabari kwa niaba ya Muungano wa Azimio bila ya Odinga, ambaye ni kiongozi wao ambapo vyama vya ODM na NARC-Kenya havikuwepo katika kongamano hilo.
Hata hivyo, alikosoa makubaliano ya viongozi wa Azimio, akisema ni sawa na kumpindua Odinga kutoka katika wadhifa wake kama kiongozi wa muungano.