Mbunge wa Gilgil nchini Kenya, Martha Wangari, amelaani vikali kile alichokiita “mauaji ya vijana wa Kenya kwa sababu ya kutoa maoni yao kuhusu serikali kupitia mitandao ya kijamii,” akisisitiza kuwa viongozi wa umma lazima wakubali kukosolewa.
Akizungumza Jumapili katika eneo la Karunga, Wangari alisema kwa mujibu wa Citizen Digital kuwa wanasiasa na watumishi wa umma hawapaswi kutarajia kuungwa mkono au kupendwa na kila mtu, bali wanapaswa kuwa tayari kuvumilia maoni tofauti.
“Nimewahi kutukanwa sana na kukosolewa Gilgil, lakini sijaenda mahakamani. Kesi hizo huchukua muda na si za msingi. Badala yake, ninachagua kusikiliza na kujifunza kwa sababu uongozi bora unatokana na mrejesho wa wananchi,” alisema.
Mbunge huyo aliongeza kuwa maofisa wa umma wanapaswa kuwa na ngozi ngumu na kwamba hali ya sasa ya vijana kuteswa au kuuawa kwa sababu ya kutumia haki yao ya kujieleza ni ya kutisha na isiyokubalika.
“Hatuwezi kuendelea kuona wanawake wakilia kila siku kwa kupoteza watoto wao kwa hali ya kikatili namna hii,” aliongeza kwa huzuni.
Wangari alisema kuwa Bunge la Taifa tayari limemuita Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, kutoa maelezo kuhusu ongezeko la visa vya mauaji ya kiholela na uonevu dhidi ya wananchi wanaokosoa serikali kupitia mitandao.
Akitetea haki ya kujieleza, Wangari pia aliwahimiza vijana kutumia uhuru huo kwa busara na kwa kuzingatia maadili.
Kisa kilichovuta hisia za wengi ni kifo cha hivi karibuni cha mwanablogu na mwalimu, Albert Ojwang’, aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi Juni 8, 2025, baada ya kukamatwa kwa madai ya kuchapisha ujumbe wa kumtusi Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Eliud Lagat. Uchunguzi wa kitabibu (post-mortem) ulionesha kuwa Ojwang’ alifariki kutokana na mateso, kinyume na madai ya polisi kwamba alijinyonga.
Mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Beatrice Elachi, ni miongoni mwa viongozi waliokosoa matumizi ya mitandao ya kijamii, hasa na vijana. Alidokeza kuwa kuna mipango ya kuwasilisha marekebisho ya Katiba kwa lengo la kudhibiti zaidi matumizi ya mitandao.
“Watu wamegeuza majukwaa kama X na Facebook kuwa maeneo ya kutukana wanasiasa na hata wenzao. Huu ni matumizi mabaya ya uhuru wa kujieleza,” alisema Elachi.
Hata hivyo, mashirika ya haki za binadamu nchini yameonya kuwa juhudi za kukandamiza mitandao zinaweza kugeuka kuwa mashambulizi dhidi ya haki za msingi kama vile uhuru wa kujieleza, kushiriki mjadala wa kisiasa na kuwawajibisha viongozi wa umma.