Latest Posts

WANASIASA WA UPINZANI BURUNDI WAPANGA KUCHUKUA SILAHA KUPINGA MATOKEO YA UCHAGUZI

Baadhi ya wanasiasa wa upinzani kutoka makundi matatu ya kisiasa yaliyoikimbia Burundi wametangaza hatua ya kuanza mapambano ya silaha wakipinga kile wanachodai kuwa ni wizi mkubwa wa kura katika uchaguzi uliofanyika nchini humo.

Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mwishoni mwa wiki hii mjini Brussels, Ubelgiji kwa mujibu wa BBC, viongozi hao wamedai kuwa matokeo ya uchaguzi huo ni haramu na kwamba juhudi zote za amani zimegonga mwamba.

Frederique Bamvuginyumvira, aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Burundi, amesema: “Tumeona uchaguzi ukiibiwa waziwazi. Watu walinyimwa haki ya kupiga kura, wengine walilazimishwa, na baadhi kunyimwa kabisa kadi za kupigia kura. Serikali inatutesa. Tumeamua kuchukua silaha kuikomboa nchi yetu.”

Bamvuginyumvira amesisitiza kuwa hatua hiyo imeamuliwa baada ya kushindwa kwa zaidi ya programu nane za mazungumzo, akisema: “Tulijaribu njia za amani, tumepuuzwa. Sasa tumeamua kupigana – si kwa chuki, bali kwa ajili ya ukombozi.”

Makundi yanayohusishwa na mpango huo ni pamoja na CFor-Arusha (Muungano wa Vikosi vya Upinzani kwa Marejesho ya Mkataba wa Arusha), CN (Coalition for the Renaissance of the Nation), inayowakilishwa na Chauvinau Mugwengezo na Patriotic Action Movement, kupitia msemaji wake Liberat Ntibashirakandi

Wanasiasa hao hawakufafanua wazi ni kundi gani litaendesha harakati hizo, lakini wamesisitiza kuwa kuna uungwaji mkono kutoka ndani na nje ya Burundi.

Tangu mwaka 2015, Burundi imeendelea kukumbwa na mivutano ya kisiasa kutokana na migogoro ya uchaguzi na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu, hali iliyosababisha baadhi ya wanasiasa na wanaharakati kukimbilia uhamishoni.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!