Latest Posts

MHARIRI AKAMATWA KWA MAKALA YA KEJELI DHIDI YA RAIS MNANGAGWA

Mhariri mashuhuri wa gazeti la Zimbabwe Independent, Faith Zaba, amekamatwa na kuzuiliwa jijini Harare siku ya Jumatano kwa kuchapisha makala ya kejeli inayomkosoa Rais Emmerson Mnangagwa, hatua ambayo imekosolewa vikali na makundi ya wanahabari na watetezi wa haki za binadamu kuwa ni shambulio dhidi ya uhuru wa kujieleza.

Zaba (55), anashitakiwa kwa kuchapisha makala yenye kichwa “When You Become a Mafia State” kupitia safu ya Muckraker, ikielezwa na upande wa mashtaka kuwa maudhui ya makala hiyo ni ya uongo, yenye lengo la kuchochea chuki za raia dhidi ya Rais huyo mwenye umri wa miaka 82.

“Yaliyomo kwenye makala hiyo si ya kweli na yamelenga kuzua hisia za uhasama kwa wananchi dhidi ya Rais,” alisema mwendesha mashtaka Takudzwa Jambawu mahakamani.

Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Harare iliagiza Zaba azuiliwe hadi Alhamisi, ambapo uamuzi wa maombi ya dhamana utatolewa.

Wakili wake, Chris Mhike, alisema ni jambo la kusikitisha kwa mteja wake kulala mahabusu kwa siku ya pili mfululizo huku akiwa na hali ya kiafya inayohitaji uangalizi. “Gereza si sehemu salama kwa mtu mwenye matatizo ya afya,” alisema Mhike.

Zaba ni mwandishi mwingine miongoni mwa waandishi kadhaa waliofikishwa mahakamani nchini humo kwa madai ya kuandika au kuripoti taarifa zinazodhoofisha mamlaka ya Rais Mnangagwa, ambaye anazidi kukosolewa kwa kushinikiza kubaki madarakani baada ya muhula wake wa sasa kukamilika mwaka 2028.

Katika tukio la awali mwaka huu, mwanahabari Blessed Mhlanga alikamatwa Februari na kushikiliwa kwa zaidi ya siku 70 baada ya kufanya mahojiano na mwanasiasa mkongwe Blessed Geza, ambaye alimkosoa Mnangagwa hadharani na kutaka ajiuzulu.

Chama cha Waandishi wa Habari Zimbabwe (ZUJ) kilitoa taarifa kikisema “kinakerwa sana na matumizi ya sheria kuwanyamazisha waandishi wa habari” na kikatoa wito wa kuachiwa mara moja kwa Faith Zaba.

“Uandishi wa kejeli, iwe ni wa ucheshi au ukosoaji, ni sehemu ya haki ya kujieleza na haupaswi kufanywa kuwa kosa la jinai,” taarifa ya ZUJ ilieleza.

Kwa upande wake, Media Alliance of Zimbabwe ilisema hatua hiyo inaonesha jinsi uhuru wa vyombo vya habari unavyoendelea kudharauliwa nchini humo.

Shirika la Reporters Without Borders limeiweka Zimbabwe katika nafasi ya 106 kati ya nchi 180 duniani katika orodha yake ya kila mwaka kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, ikiwa ni dalili ya kuporomoka kwa mazingira salama kwa waandishi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!