Huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu kwa taifa letu kama inavyotaka katiba yetu. Nchi yetu ni waakti inapata uhuru ilikuwa ina mfumo wa chama kimoja cha siasa mpaka mwaka 1992 ilipoamua kubadili na kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi.
Bila shaka katika chaguzi zote kuanzia mwaka 1995 hakuna uchaguzi ulikuwa wa kuvutia zaidi na wenye nguvu ya aina yake kama uchaguzi wa mwaka 2015. Hii haimaanishi chaguzi zingine hazikuvutia lah hasha ila wa 2015 ulikuwa wa kipekee, na upekee wake uliletwa na upinzani wa wagombea wawili Hayati Dkt. John pombe Magufuli wa CCM na Hayati Edward Lowasa akiwakilisha UKAWA japokuwa kwenye Urais kura alipiogiwa kura kama CHADEMA.
Tuachane na historia za wagombea na ukubwa wao tuangalie nafasi za vyama vya upinzani. Kwanza mwaka huu mpaka kufikia mwezi wa pili chama kikuu cha upinzani nchini (CHADEMA) kilikuwa kimefanya mchakato wa ndani wa kumpata mgombea Urais ambaye alikuwa ni Dkt. Wilbroad Slaa. Ulipokuja kupatikana Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambayo ilikuwa ni muunganiko wa CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD mgombea Urais akawa ni mmoja ambaye ni Lowassa huku kwenye majimbo wakigawana kutokana na ushawishi wachama na eneo husika.
Nini ilikuwa faida ya UKAWA?
Kwanza wanavyama wa vyama vikubwa wote walikuwa wanapiga kura kwa mgombea mmoja ambaye ni Lowassa. Pili wabunge na madiwani walinadiwa na watu wenye ushawishi kutoka vyama hivyo vitatu hivyo hapakuwa na mgawanyiko wa kura. Matokeo ya Urais mwaka huo hayati Magufuli alipata kura 8,882,935, sawa na asilimia 58.46% na Lowassa alipata kura 6,072,848, sawa na asilimia 39.97%. wabunge wa upinzani walikuwa zaidi ya 100 huku wabunge wa CCM wakiwa zaidi ya 250.
Sasa mwaka huu imebaki miezi mitatu vyama vya upinzani ndiyo kwanza vinasagiana kunguni na wananchi wamebaki njia panda wamuamini anayesema anataka mabadiliko au anayesema ana madai sita lakini atashiriki na atalinda kura ‘bila kumsusia mhuni’ au yule anayesema anaendelea alipoishia.
Ni kweli lengo namba moja la chama chochote cha upinzani ni kushika dola na ni sahihi kuwa na njia yake na mbinu zake ili kushika dola. Chama kikuu cha upinzani ambacho ni CHADEMA kimesema kama hakuna mabadiliko hakutakuwa na uchaguzi (No reforms no election) na wamesimamia msimamo huo mpaka sasa pamoja na changamoto wanazokumbana nazo. Na ili kuthibitisha hawaridhiki na michakato ya uchaguzi wamekataa kusaini maadili ya uchaguzi.
Vyama vingine vilisaini maadili ya uchaguzi ikiwemo ACT Wazalendo. Lakini hivi karibuni ni kama hivi vyama pinzani hasa CHADEMA, ACT na CHAUMMA wamekuwa wakirushiana maneno mpaka unajiuliza wametupiwa jinamizi la kugombana?.
Waswahili walisema vita vya panzi furaha kwa kunguru, saaa hivi upinzani wakishughulikiana CCM anafurahia kwa sababu yeye mchakato wake wa uchaguzi utakuwa mgumu ndani tu jambo ambalo analimudu lakini akija kwenye kunadi sera na kupambana huku nje ni kama hatakutana na upinzani wenye nguvu.
Wakati wa nyuma CHADEMA ilijibebea umaarufu na kuaminika na wananchi wengi kupitia kukosoa CCM kutangaza madhaifu ya serikali, kukosoa, na kufanya mikutano mikubwa ya kueleza yale ambayo hayafai ndani ya serikali. Unakumbuka mkutano wa hadhara wa Mwembeyanga uliotaja ufisadi ndani ya serikali maarufu kama list of shame?.
WanaCHADEMA wanasema anayesema atalinda kura ni ‘TAPELI’ na ACT anasema anayekuambia atazuia uchaguzi ni ‘tapeli’. CHADEMA kila siku wapo X(zamani twitter) kuwakosoa ACT Wazalendo na ACT wapo X na majukwaani kujibu hoja za CHADEMA. Cha kushangaza wamefikia mahali upinzani wanaitana ‘TAKATAKA’ hahahaha hii ni maajabu.
Upinzani amkeni ni muda wa kuungana sio kupingana na kutukanana. Kama lengo lenu ni dola aliyeshika dola ni CCM pambaneni naye sio upinzani mwenzenu kaeni jadilianeni kukabiliana na CCM la sivyo mnaipa urahisi CCM kupenya kwenye uchaguzi