Rais wa Ukraine, Volodymry Zelensky, ametangaza nchi yake na Urusi zitafanya mazungumzo mapya ya kutafuta amani, ikiwa ni muendelezo wa awamu mbili za awali za mazungumzo ambayo hayakuzaa matunda.
Kwa mujibu wa msemaji wa Serikali ya Ukraine, mazungumzo haya yatafanyika Ankara, katika eneo lilelile walilofanyia mazungumzo ya mwezi Mei na June.
Aidha wakati huu Rais wa Marekani, Donald Trump akiongeza shinikizo kwa Urusi kwa kuipa siku 50 kukubali mpango wake wa amani ama iwekewe vikwazo, Tangazo la Zelensky limekuja saa chache tangu Kremlini ioneshe kutokuwa tayari na mpango wowote wa amani.
Tangazo la Kiev pia limekuja wakati ambapo, Urusi imezidisha mashambulio katika miji mbalimbali ya nchi hiyo, mashambulio ambayo yaliharibu miundombinu na kugharimu maisha ya watu.
Wakati huu Ukraine ikionesha kuwa tayari, Moscow haijazungumzia chochote kuhusu tangazo la Kiev, ingawa watu wa karibu na mchakato unaoendelea, wanasema huenda mazungumzo yakajikita tena katika kubadilishana wafungwa na uwezekano wa mkutano wa ana kwa ana kati ya Putin na Zelensky.