Mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine yaliyofanyika jana jijini Istanbul yalijikita zaidi katika mpango wa kubadilishana wafungwa wa kivita. Kikao hicho kilichodumu kwa takriban dakika 40 hakikuweza kufikia makubaliano ya wazi kuhusu kusitisha mapigano au uwezekano wa kukutana ana kwa ana kati ya viongozi wa nchi hizo mbili.
Kuwa mujibu wa taarifa ya DW, mkuu wa ujumbe wa Ukraine, Rustem Umerov, ameeleza kuwa taifa lake limependekeza kufanyika kwa mkutano kati ya Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine na Rais Vladimir Putin wa Urusi kabla ya mwisho wa mwezi Agosti.
Umerov amedai kuwa iwapo Urusi itakubali pendekezo hilo, hiyo itakuwa ishara ya nia njema kuelekea kumaliza vita.
Hata hivyo, mkuu wa ujumbe wa Urusi Vladimir Medinskiy amesema mkutano wa moja kwa moja kati ya viongozi hao haupaswi kuwa kwa ajili ya majadiliano ya awali, bali uwe wakati wa kusaini makubaliano ya amani ya mwisho.
Ametoa msimamo kuwa Urusi inatafuta usitishwaji mapigano wa muda mfupi masaa 24 hadi 48 wakati Ukraine inasisitiza usitishwaji wa muda mrefu na wa mara moja.