Latest Posts

SIKU YA VIJANA KIMATAIFA 2025: UZOEFU, UBUNIFU NA UONGOZI WA VIJANA KWA MITANDAO SALAMA NA JUMUISHI TANZANIA

Duniani kote, karibu asilimia 80 ya vijana (takribani bilioni 1.9 wenye umri wa miaka 15-24) wanatumia intaneti, hii ikiwa ni asilimia 15 zaidi ya wastani wa watumiaji wa asilimia 65. Kadri

matumizi ya mitandao yanavyozidi kuongezeka, ndivyo pia washukiwa wa ukatili na unyanyasaji mtandaoni wanavyozidi kuongezeka. Ukatili wa kijinsia unaowezeshwa na teknolojia (TFGBV) ni aina ya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana unaotekelezwa kwa kutumia aina yoyote ya

teknolojia ikiwemo simu, kompyuta, mitandao ya kijamii au vyombo vya habari vya kidijitali. Huu ni ukiukwaji wa faragha, heshima, uhuru wa mtu na unaweza kuwa na athari mbaya sana. Hisia za hofu, wasiwasi, kupoteza kujiamini na hali ya kujihisi mnyonge ni za halisi na hudumu kwa muda mrefu.

TFGBV imeshamiri duniani kote, ikiwa na kiwango cha juu cha asilimia 38, kwa mujibu wa ripoti ya The Economist Intelligence Unit (EIU) – hii ni sawa na karibu wanawake wawili kati ya watano.

EIU inaripoti kuwa asilimia 85 ya wanawake na wasichana waliopo mtandaoni wamewahi

kushuhudia aina fulani ya ukatili mtandaoni ukifanywa dhidi ya wanawake na wasichana wengine, Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Idadi ya Watu latanabaisha (UNFPA, 2021).

Zaidi ya nusu, yaani asilimia 58 ya wasichana na wanawake vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 25 wamewahi kupitia unyanyasaji wa mtandaoni katika nchi 22 duniani ikiwemo Tanzania. Vijana ndio kundi kubwa lililo hatarini zaidi kulengwa na TFGBV kwa misingi ya utambulisho wao kama vile jinsia zao, namna wanavyojieleza kijinsia, umri wao, itikadi zao au mwelekeo wao wa kijinsia.

Kukabiliana na TFGBV kama changamoto inayokua kwa kasi ni suala muhimu sana, si jambo la hiari tena.

Teknolojia ina mchango mkubwa kwenye ajenda za maendeleo lakini pia ina hatari nyingi na madhara makubwa. Ili kufanya majukwaa yote ya mtandaoni yawe salama na jumuishi, tunahitaji kwanza kuelewa vyema jinsi teknolojia inavyoathiri maisha yetu, hasa vijana.

Je, manufaa ya Teknolojia ni yapi?

Kama kizazi kilichozaliwa kwenye ulimwengu wa kidijitali, vijana wana nafasi kubwa ya kutumia fursa nyingi zinazotokana na teknolojia ili kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi na yenye usawa.

Teknolojia ni moja ya nyenzo bora zaidi za jamii katika kupunguza ukosefu wa usawa: Hufungua milango kwa vijana katika nyanja za elimu, ajira, biashara na ushiriki wa kiraia na inaweza kukuza usawa wa kijinsia na amani kupitia ubunifu na kubadilishana uzoefu. Teknolojia salama zinaweza kuboresha upatikanaji wa taarifa, huduma bora za afya ya uzazi na afya ya akili kwa vijana balehe na vijana kwa ujumla, na hivyo kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi kwa taarifa sahihi.

Kwenye upatikanaji wa elimu na maarifa kidijitali, turejee nyuma kidogo katika historia ya

Elimika Wikiendi, kutoka kiunganishi cha mtandaoni kwa kimombo hashtag hadi jukwaa

namba moja la elimu kwa njia ya mtandao nchini Tanzania, tena kwa lugha ya Kiswahili, na sasa taasisi ya elimu ya usalama mtandaoni inayounga mkono maendeleo ya vijana Tanzania.

Kwa zaidi ya miaka nane, Elimika Wikiendi kupitia jukwaa lake la elimu mtandaoni almaarufu #ElimikaWikiendi, imetumia fursa na ubunifu unaowezeshwa na maendeleo ya teknolojia kugeuza mitandao ya kijamii kama vile X (Zamani Twitter), Facebook, Instagram na TikTok kuwa kitovu cha elimu na maarifa kwa vijana.

Kila wikiendi, maudhui ya elimu jukwaani hufikiwa na zaidi ya watu milioni mbili mtandaoni, huku ufikaji wa kila mwezi ukizidi watu milioni nane kutoka Tanzania na nje ya nchi. Elimika Wikiendi

imegusa maisha ya maelfu ya vijana kupitia teknolojia, ambapo zaidi ya vijana 1000

wameunganishwa na fursa mbalimbali kutokana na elimu inayotolewa na wataalamu kupitia vipindi vyetu jukwaani, zaidi ya vijana 200 wameanzisha biashara mtandaoni na nje ya mtandao kutokana na maarifa waliyopata kupitia kongamano letu la mwaka la #FursaKwaVijana na lile la

mafunzo ya ana kwa ana la Nikonekt, huku vijana 130 wakijiunga na mtandao wa wahamasishaji wa masuala ya kijamii mtandaoni, watengeneza maudhui na wanaharakati wa haki za kidijitali tuliouasisi. Yote hayo, yamefanyika kutokana na manufaa ya teknolojia, kutumia mitandao ya kijamii kama daraja la fursa, elimu, uchechemuzi na upatikanaji wa taarifa sahihi miongoni mwa vijana.

 

Je, changamoto za teknolojia ni zipi?

Maendeleo ya kiteknolojia pia yanachangia kuongezeka kwa mgawanyiko wa kidijitali na kutokuwepo kwa usawa wa kijamii.

Takribani theluthi mbili ya vijana na watoto walio chini ya umri wa miaka 25 hawawezi kufikia intaneti wakiwa nyumbani, changamoto kama vile kushindwa kumudu gharama za intaneti kutokana na umaskini, ufikiaji usio kasi wa miundombinu ya intaneti maeneo yasiyofikika kirahisi hasa vijijini pamoja na kuhama hama makazi huchangia zaidi katika kuzorotesha upatikanaji huo.

Wasichana balehe, hasa wale wanaotoka katika kaya masikini zaidi, ndio walio katika nafasi

ndogo zaidi ya kuweza kuunganishwa mtandaoni. Pengo hili lina maana kwamba, mamilioni ya vijana hawawezi kupata elimu na ujuzi wa kidijitali wanaohitaji ili kufanikiwa na kufikia uwezo wao kamili kwenye ulimwengu wa kidijitali unaobadilika kwa kasi.

Aidha, kwa kuwa majukwaa ya kidijitali kama vile mitandao ya kijamii mara nyingi haina udhibiti wa kutosha na haisimamiwi ipasavyo, maudhui hatarishi hupakiwa na kusambazwa, mitandao ya kijamii pia imejaa maneno ya chuki, hususan dhidi ya wasichana na wanawake. Hali hii huwaweka vijana, hasa wasichana balehe katika hatari kubwa ya ukatili wa kijinsia unaowezeshwa na teknolojia (TFGBV).

Hali hii inaweza kuwa na madhara makubwa kwa afya ya mwili na akili ya vijana na huathiri kwa namna tofauti wasichana na wavulana — kwa wavulana (kuwa na mwelekeo wa kutumia nguvu, msimamo mkali, chuki dhidi ya wasichana na upatikanaji rahisi wa maudhui yasiyo na maadili ambayo huathiri vibaya mtazamo wao kuhusu mahusiano yao na jamii) na kwa wasichana (hali ya kushinikizwa na muonekano wa nje, hofu, kunyamazishwa, kupoteza kujiamini na kujihisi unyonge).

Shuleni, ulimwengu wa teknolojia unaleta hatari kubwa kwa vijana wadogo. Uonevu mtandaoni (cyberbulling) ni tatizo linalokua kwa kasi, likimuathiri mtoto 1 kati ya 10. Tunajua kwamba

ukatili katika aina zake zote unaweza kuwa na athari mbaya na za muda mrefu kwa afya ya mwili na akili ya vijana shuleni na hivyo kuathiri maendeleo yao ya elimu. Kwa sababu ya athari zake

katika ujifunzaji, ukatili shuleni ikiwa ni pamoja na uonevu mtandaoni si suala la haki za watoto pekee. Una gharama kubwa kwa mifumo ya upatikanaji wa elimu iwapo hautashughulikiwa.

Kwenye nchi kama Tanzania ambayo zaidi ya 77% ya watu wake wana umri chini ya miaka 35 na idadi ya watumiaji wa intaneti ikifikia milioni 49, huku ikitarajiwa kuongezeka mara mbili ifikapo 2030. Hii ni fursa kubwa, lakini pia ni changamoto kubwa zaidi hususan kwa vijana.

ELIMIKA WIKIENDI inafanya nini?

Elimika Wikiendi inafanya kazi kubwa kuhakikisha majukwaa ya mtandaoni ni jumuishi, salama na huru dhidi ya ukatili, hasa kwa vijana kupitia;

Kukuza uelewa kuhusu ukatili wa kijinsia unaowezeshwa na teknolojia (TFGVB) ikiwemo uonevu mtandaoni (cyberbulling) na unyanyasaji mtandaoni (online harassment) na kuhamasisha jamii kupitia kampeni za kibunifu na mijadala ya elimu ndani na nje ya mtandao (kama vile

#ElimikaWikiendi), tukikuza maarifa na uwezo wa vijana katika kuufanya ulimwengu halisi na wa kidijitali kuwa wa haki, usawa, amani na usalama huku wakitambua mustakabali wa dunia salama kwa wote uko mikononi mwao.

Kwa kutambua kuwa idadi kubwa ya washukiwa wa ukatili wa kijinsia mtandaoni ni wanaume na wavulana na wengi wa waathirika na manusura ni wanawake na wasichana, Elimika Wikiendi ina mikakati maalum iliyobuniwa kufanya kazi na wanaume na wavulana ili kuhamasisha tabia

chanya mtandaoni na kuwajengea uwezo wanawake na wasichana kupitia mafunzo ya usalama mtandaoni.

Elimika Wikiendi inatoa mafunzo ya ujuzi wa kidijitali ikiwemo usalama mtandaoni kwa vijana

hasa wasichana shuleni na vyuoni, ili kusudi watumie teknolojia kufikia uwezo wao kamili katika ulimwengu wa kidijitali huku tukiwawezesha kutambua hatari za mtandaoni kama vile ukatili wa kijinsia unawezeshwa na teknolojia na hatua wanazoweza kuchukua.

Pia, tunatumia jukwaa letu la mtandaoni lenye nguvu na ushawishi kuwawezesha waathirika wa ukatili wa kijinsia mtandaoni kupaza sauti zao, kuchukua hatua kuripoti matukio na kuwaunganisha na msaada wa kijinsia, kisheria na kisaikojia kutoka kwa wataalamu.

Vilevile, Elimika Wikiendi inawajengea uwezo walimu, wazazi, walezi na watoa huduma kupitia mafunzo ya usalama mtandaoni ili waweze kuwasaidia vijana kwa ufanisi zaidi katika safari yao ya kidijitali. Mafunzo haya yanawawezesha kuelewa mazingira ya majukwaa ya kidijitali, kutambua

viashiria vya hatari mtandaoni na kutoa msaada wa haraka pale inapohitajika. Kupitia ushirikiano huu wa kielimu na kijamii, Elimika Wikiendi inalenga kujenga kizazi salama, chenye maarifa na

uwezo wa kutumia teknolojia kwa tija, ubunifu na kwa namna inayochochea maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.

Elimika Wikiendi pia inafanya uchechemuzi wa sheria za ulinzi na usalama mtandaoni nchini

Tanzania na miongozo mbalimbali ya kimataifa. Katika eneo hili, tunahimiza watunga sera kufanya mapitio ya sheria mbalimbali za ulinzi na usalama mtandaoni kama vile Sheria ya Makosa ya

Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 pamoja na sera, kanuni na miongozi mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, ili kuzuia ukatili wa kijinsia unaowezeshwa na teknolojia.

 

Nini kinahitajika ili kuhakikisha majukwaa ya mtandaoni yanabaki salama?

Kwa uzoefu wetu wa miaka kumi ya uendeshaji wa jukwaa la elimu kwa njia ya mtandao, Elimika Wikiendi inatambua juhudi za serikali na mashirika mbalimbali yanayofanya kazi kubwa ya kulinda majukwaa ya mtandaoni ili yawe salama na jumuishi. Hata hivyo, bado kunahitajika juhudi za

pamoja na za haraka zaidi kudhibiti ukatili wa kijinsia mtandaoni zitakazoendana na kasi ya

maendeleo ya teknolojia mpya kama vile akili unde, ili kuhakikisha majukwaa yote ya mtandaoni ni salama na jumuishi kwa watumiaji wote wa mtandao wakiwemo vijana. Teknolojia ni chombo. Vijana wanahitaji msaada kila upande ili kuhakikisha kuwa inatumika kwa njia inayokuza heshima, utu na haki za binadamu kwa watu wote, katika utofauti wao wote.

Rai yetu tunapoadhimisha Siku ya Vijana Kimataifa 2025 ni, mustakabali wa majukwaa salama ya mtandaoni uko mikononi mwa vijana. Vijana wana uwezo wa kuufanya ulimwengu wa kidijitali na ulimwengu halisi kuwa jumuishi zaidi, wenye haki, amani na usalama. Kama wahamasishaji wa mtandaoni, watengeneza maudhui, wanaharakati wa kidijitali na raia wema wa kidijitali, vijana

wanaweza kutumia teknolojia kuelimisha jamii kuhusu ukatili wa kijinsia mtandaoni na madhara yake kwa afya ya akili na mwili, kudai uwajibikaji, kuhamasisha maendeleo, kufichua maovu, kupinga upotoshaji na kusimama dhidi ya ubaguzi.

Pia, wanaweza kuongoza mapambano ya kudai haki za kidijitali na kulaani sheria zisizo na meno zinazoshindwa kuzuia ukatili wa kijinsia mtandaoni.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!