Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, amedai kuwa madai ya kuunganisha mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ni tishio kwa uhuru wa uchaguzi Tanzania.
Akizungumza Jumatano Agosti 27, 2025 katika mkutano wa hadhara wa mtandaoni unaoitwa ‘Baraza la Kidigitali’, Mnyika amesema kuwa muunganiko huo unazua mashaka makubwa kuhusu usalama wa daftari la kudumu la wapigakura na uwezekano wa kuingiliwa kwa mifumo ya uchaguzi na mamlaka za serikali.
Mnyika ameeleza kuwa tangu mwaka 2005, CHADEMA imekuwa ikipinga wazo la kuunganisha mfumo wa vitambulisho vya uraia na daftari la wapigakura, akisisitiza kuwa mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA) ni chombo cha serikali ambacho hakina uhuru wa kikatiba kama INEC inavyopaswa kuwa akisema kuwa kuunganisha mifumo ya NIDA na INEC kunamaanisha daftari la wapigakura linakuwa chini ya mamlaka ya serikali badala ya tume huru, jambo linalokiuka misingi ya demokrasia.
“Mjadala huu ulianza tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2020 ambapo ulikuwa na nguvu juu ya kinachoitwa kuunganisha mfumo wa NIDA, mfumo wa vitambulisho vya uraia na mfumo wa daftari la kudumu la wapigakura unaoaminiwa na INEC. Yalipotoka haya madai sisi wengine tulionesha mashaka yetu kwamba kuunganisha hii mifumo miwili yani mfumo wa NIDA na mfumo wa tume ya taifa ya uchaguzi NEC hatua hizi zitasababisha mianya ya mifumo ya uchaguzi kuingiliwa na kutumika na mifumo ya kiserikali” amesema Mnyika.
Sambamba na hayo Mnyika amesema madai ya kuunganisha daftari la kudumu la wapigakura na mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA) kwenye uchaguzi yalianza tangu mwaka 2015, na sasa yanathibitishwa na kauli na kiongozi wa zamani wa CCM Humphrey Polepole, aliyewahi kuwa kada wa CCM, ambaye amekiri hadharani kuhusu matumizi ya daftari hilo katika kuvuruga uchaguzi.
Hata hivyo kauli ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, kwamba mifumo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imeunganishwa na ile ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imewafanya wakuu wa taasisi hizo kujitokeza hadharani na kukanusha vikali madai hayo.
wakuu hao wamesema wazi kuwa hakuna mfumo wowote wa taasisi zao uliofungamanishwa na chama chochote cha siasa, na kwamba kama jambo hilo lingekuwepo lingejulikana kwa urahisi.
Polepole, akizungumza usiku wa manane Agosti 22, 2025, alidai mifumo hiyo imekuwa chombo cha CCM kujihakikishia ushindi wa uchaguzi. Aalisisitiza kuwa wakati mifumo hiyo ikiundwa dhamira yake ilikuwa njema, lakini “ikishikwa na watu wabaya, dhamira yake ni mbaya kabisa.”
Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, alisema madai ya Polepole hayana ukweli wowote. “Hakuna kitu kama hicho. Ni vema akawaelezea vizuri labda yeye anajua na kama ameshafanya kazi Nida,” aliesema Kaji.
Nayo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilikanusha taarifa zinazodai kuwa mfumo wa uchaguzi unaotumika na Tume hiyo umeunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na chama cha siasa, hususan Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na madai kwamba zoezi la upigaji kura tayari limefanyika.
Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima kupitia taarifa ya INEC ya Agosti 23, 2025, alisema taarifa hizo zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii ni za uongo na upotoshaji zenye lengo la kupotosha umma na kuibua taharuki.
“Daftari la Kudumu la Wapiga Kura halijaunganishwa na mfumo wowote wa Serikali au wa Taasisi binafsi kwa madhumuni ya upigaji kura”, alisema Kailima.
Kailima alibainisha kuwa Tanzania haitumii mfumo wa kielektroniki katika kupiga kura, kuhesabu kura, au kutangaza matokeo. Badala yake, zoezi hilo hufanyika kwa kutumia utaratibu wa kawaida (manual).
“Ifahamike kuwa, Kitambulisho cha Taifa hakitumiki kupigia kura, bali Kadi ya mpiga kura pekee iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na kuhakikiwa ndiyo inayotumika wakati wa upigaji kura katika vituo vya kupigia kura”, alisisitiza.
Aliongeza kuwa vyama vya siasa vilishapewa Daftari la Wapiga Kura baada ya zoezi la uboreshaji kukamilika, na mawakala wa vyama watatumia daftari hilo kutambua wapiga kura siku ya uchaguzi.
Mnyika amesisitiza kuwa bila mageuzi ya kweli, hususan katika daftari la wapigakura na katiba ya nchi,Tanzania haiwezi kuwa na uchaguzi wa haki.
Katika hatua nyingine, Mnyika ametoa wito kwa serikali kuandikisha upya daftari la kudumu la wapigakura, akisema ni moja ya madai muhimu ya mageuzi ya kisiasa nchini Tanzania. Amesisitiza kuwa daftari hilo limekuwa likitumiwa kama nyenzo ya kuvuruga uchaguzi kwa miaka mingi, na kwamba mabadiliko ya msingi yanahitajika ili kuhakikisha haki na uwazi katika chaguzi zijazo.
Mnyika ameeleza kuwa udhaifu wa mfumo wa uchaguzi unatokana na kasoro za kikatiba na uunganishaji wa mifumo ya NIDA na INEC, jambo linaloathiri uhuru wa tume ya uchaguzi.
“Mimi naamini haya madai yana uzito mkubwa na hatua inabidi zichukuliwe za kuyashughulikia. Wakati umefika sasa wa kusema imetosha, tutake reforms na tuendelee na msimamo wa no reforms, no election kwamba tunataka uchaguzi uwe wa haki Tanzania,” aMEsema Mnyika kwa msisitizo.
Chama hicho kimesisitiza kuwa bila mageuzi ya kweli, hususan katika daftari la wapigakura na katiba ya nchi, Tanzania haiwezi kuwa na uchaguzi wa haki. CHADEMA inaendelea kushinikiza mchakato wa katiba mpya na uhuru wa tume ya uchaguzi kama msingi wa demokrasia ya kweli.