Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma, imeamuru mwanachama wa ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, aruhusiwe kuendelea na mchakato wa kurejesha fomu ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mahakama imeeleza kuwa zuio lililowekwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kumzuia kurejesha fomu na kumnyima nafasi ya kusikilizwa, lilikuwa kinyume cha sheria na Katiba.
Kwa mujibu wa uamuzi uliotolewa leo, Septemba 11, 2025, katika shauri Na. 21692/2025 lililofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa ACT Wazalendo pamoja na Luhaga Mpina dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mahakama imebainisha kuwa uamuzi wa Tume uliofanyika Agosti 27, 2025 uliwaathiri waleta maombi, hivyo wanapaswa kupewa fursa ya kurejesha fomu haraka.
Hata hivyo, ombi la waleta maombi la kutaka kulipwa fidia ya shilingi milioni 100 lilikataliwa na Mahakama.
Uamuzi huo umesomwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Abdi Kagomba.