Shirika la Afya Duniani (WHO) limeanza kutoa chanjo ya Ebola kwa wafanyakazi wa afya na watu waliokuwa na mawasiliano ya karibu na wagonjwa waliothibitishwa katika Jimbo la Kasai, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kutokana na mlipuko mpya wa ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa WHO, dozi 400 za awali za chanjo ya Ervebo Ebola kutoka akiba ya dozi 2,000 zilizopo nchini humo tayari zimefikishwa katika eneo la Bulape, kitovu cha mlipuko huo.
Aidha, Kundi la Kimataifa la Kuratibu Utoaji wa Chanjo limeidhinisha kutumwa kwa dozi 45,000 za ziada za chanjo ili kusaidia kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo; hii ni kwa mujibu wa kituo cha habari cha BBC
Huu ni mlipuko wa kwanza wa Ebola kuripotiwa nchini DRC katika kipindi cha miaka mitatu, na ulitangazwa mapema mwezi Septemba. Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya mjini Kinshasa zinaonesha kuwa hadi sasa kuna visa 32 vinavyoshukiwa, kati ya hivyo 20 vimebainishwa rasmi, huku vifo 16 vikiripotiwa.
Misitu minene ya kitropiki ya Congo inajulikana kama hifadhi ya asili ya virusi vya Ebola, vinavyosababisha homa kali, maumivu ya mwili, kuharisha, na vinaweza kubaki mwilini mwa walionusurika kwa miaka kadhaa kabla ya kujitokeza tena.
Meneja wa Eneo la Mpango wa WHO, Patrick Otim, aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva wiki iliyopita kuwa hatua za haraka zinaweza kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.
“Kudhibiti mlipuko huu inawezekana, lakini itakuwa changamoto ikiwa tutakosa fursa hii,” alisema Otim, akitoa wito wa msaada zaidi kutoka kwa serikali ya Congo na washirika wa kimataifa.