Bunge la Chad limepitisha marekebisho ya katiba yatakayomruhusu Rais wa nchi hiyo kuongeza muda wa kukaa madarakani kutoka miaka 5 hadi 7, huku mabadiliko hayo yakiwa hayana kikomo cha mihula.
Kwa mujibu wa taarifa ya Radio France Internationale (RFI) iliyochapishwa Jumanne Septemba 16, 2025, hatua hiyo ilifikiwa Jumatatu Septemba 15, mara baada ya kusainiwa kwa pendekezo la marekebisho ya katiba yanayompa Rais mamlaka ya kuendelea kuongoza kwa kipindi kisicho na kikomo.
Muswada huo uliwasilishwa na muungano wa chama tawala Patriotic Salvation Movement (PSM), ukifanyia marekebisho vipengele vya katiba iliyopitishwa mwezi Desemba 2023. Katika kura ya wabunge, jumla ya wabunge 171 waliunga mkono mabadiliko hayo.
Baada ya hatua hiyo, muswada huo unatarajiwa kupelekwa katika Bunge la Seneti ili kupata kura za mwisho za kuidhinisha rasmi marekebisho mapya ya katiba.