Na; mwandishi wetu
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Viktoria kupitia kwa Katibu wake Zacharia Obadi kimedai kuwa Makamu Mwenyekiti wake wa Kanda Khalid S. Hussein amekamatwa na Jeshi la Polisi Oktoba 02.2025
Taarifa za madai ya kukamatwa kwa kiongozi huyo zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii hususani kwenye makundi ya Whatsapp kupitia taarifa iliyokuwa imetolewa na Zacharia Obadi, ambapo taarifa hiyo ilidai kuwa kiongozi huo amekamatwa akituhumiwa kutaka kushusha ‘mabango ya kampeni’ ya mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan
Mapema leo, Ijumaa ya Oktoba 03.2025 baada ya kuona taarifa hiyo, Jambo TV imemtafuta Zacharia Obadi ambaye amethibisha kuwa taarifa iliyopo mitandaoni ni yake na kuongeza kuwa, Makamu Mwenyekiti huyo amekamatiwa wilayani Muleba na baadaye usiku alisafirishwa kuelekea Bukoba, mkoani Kagera
“Tumeshatuma viongozi wetu wa Kagera wafuatilie, kwa sababu hatua iliyopo sasa hivi ni kufanya utaratibu wa kumdhamini, lakini pia tumetoa wito kwa Jeshi la Polisi maana hii kamata kamata imeanzia Mwanza, watu wamekamatwa, hata wale wanaoenda kutoa huduma za msingi kwa watu waliokamatwa na wao wanakamatwa, kwahiyo kuna kamata kamata ambayo jaina msingi wowote na kwakweli inachochea chuki tu kwa Watanzania” -Obadi
Jambo TV imezungumza na Katibu wa CHADEMA mkoa wa Kagera Daniel Damian ambapo ameeleza kuwa usiku walipokea taarifa ya kukamatwa kwa kiongozi huyo na kupitia taarifa hiyo wakaelezwa kuwa mtuhumiwa amefikishwa kwenye Kituo cha Polisi Bukoba, lakini mapema leo asubuhi yeye binafsi (Katibu wa CHADEMA mkoa wa Kagera) amefika kituoni hapo na kuelezwa kuwa mtu huyo hajafikishwa kituoni hapo
Alipoulizwa kama wana uhakika gani wa kwamba kiongozi huyo amekamatwa na Jeshi la Polisi, Katibu huyo wa CHADEMA mkoa wa Kagera amesema wamepata taarifa kutoka kwenye chanzo chao cha kuaminika ambacho hata hivyo hakutaka kukiweka wazi kupitia mazungumzo hayo
“Tuna uhakika kwamba amekamatwa na Polisi kwa sababu aliyetupatia taarifa ni mtu wa hapohapo, hatuwezi kutaja jina lake kwa sasa, lakini leo nimefika, nilikuwa kwa OCD mimi mwenyewe na kuelezwa kuwa hajaletwa, kwa sasa tunaendelea kufuatilia ili tujuwe mahala alipo” -Daniel
Ili kupata uthibitisho wa madai hayo, mapema asubuhi ya leo Jambo TV ilianza jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera kwa njia ya simu, ambapo awali simu yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyeeleza kuwa Kamanda alikuwa kwenye kikao wakati huo, hivyo atafutwe baada ya saa kadhaa
Baadaye tena, tulipopiga simu hiyo, bahati iliyoje alipokea mwenyewe Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera SACP Blasius Chatanda ambapo alipoulizwa kuhusu suala hilo alijibu kuwa kwa wakati huo yuko nje ya ofisini, na kwamba pindi akirejea ofisini na kupata taarifa ataturejea kutupatia
“Niko nje ya ofisi, ngoja nifuatilie nijuwe ofisini kuna nini, na kama lipo limefikia wapi, maana nilikuwa nimetoka kidogo, nikipata taarifa ya kina nitakujulisha, mimi nikishakuwa tayari nitakupigia mwenyewe” -SACP Chatanda.