Latest Posts

PROF. ANANGISYE: MRADI WA HEET NI UKURASA MPYA KATIKA HISTORIA YA ELIMU NCHINI

 

 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye, amesema kuwa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET – Higher Education for Economic Transformation) ni hatua muhimu na ya kihistoria katika kubadilisha mfumo wa elimu ya juu nchini Tanzania, kutoka mfumo wa kawaida wa kitaaluma hadi kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa viwanda na uendelevu wa taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumanne Oktoba 21, 2025, katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari, Profesa Anangisye amesema mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ufadhili wa Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 425, umelenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kuhuisha mitaala ili iendane na soko la ajira.

Amesema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimepata jumla ya Dola za Kimarekani milioni 49.5 (sawa na shilingi bilioni 121) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Julai 2021 hadi Juni 2026, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 80 na kubainisha kuwa fedha hizo zimewezesha ujenzi wa miundombinu ya kisasa, ikiwemo madarasa, maabara, karakana, na hosteli za wanafunzi.

Ameongeza kwa kusema kuwa, mradi huo umeimarisha matumizi ya teknolojia katika kufundisha na kujifunza, ambapo zaidi ya wanafunzi 39,000 na wahadhiri 600 wameingizwa katika mfumo wa masomo ya kidijitali, huku masomo 1,000 yakiwa tayari yameingizwa kwenye mfumo wa e-learning. Aidha, wahadhiri 377 wamepata mafunzo ya namna ya kutumia teknolojia ya kujifunzia kwa njia ya mtandao kupitia Kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (CVL).

Kupitia HEET, UDSM pia imeboresha mitaala 250 ili iendane na mahitaji ya soko la ajira na kuongeza muda wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi ambapo pia mabadiliko hayo yanatekeleza dira ya taifa ya maendeleo ya 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi wa viwanda unaoongozwa na maarifa, ubunifu na teknolojia.

Katika uendelezaji wa rasilimali watu, Profesa Anangisye amesema kuwa wanataaluma 29 wamefadhiliwa kusomea Shahada za Uzamivu na Umahiri katika vyuo vikuu vinavyotambulika kimataifa, lengo likiwa ni kuongeza uwezo wa kufundisha, kufanya tafiti na kuendeleza ubunifu ndani ya chuo. Pia, chuo kimeanzisha ofisi maalum ya ushirikiano na sekta binafsi na Kamati za Ushauri za Kitasnia, hatua ambayo imeongeza ajira kwa wahitimu na uhusiano wa karibu na viwanda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amepongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa usimamizi mzuri wa mradi huo, akisema majengo yanayojengwa yanaonesha kiwango kikubwa cha utaalamu na ubunifu.

“Leo tumeshuhudia majengo makubwa na mazuri yanayojengwa hapa UDSM kupitia mradi wa HEET. Nawapongeza kwa uhandisi mzuri na usimamizi bora. Vyombo vya habari tutaendeleza ajenda ya ubunifu wa chuo hiki na kuujulisha umma,” alisema Balile.

Balile pia amewataka Watanzania kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa amani wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 kwa kusema

“Wiki ijayo tunapiga kura, chagueni viongozi mnaowataka, kura yako ndiyo itakayohesabika, siyo vurugu.”

Profesa Anangisye amehitimisha kwa kusema kuwa Mradi wa HEET ni ukurasa mpya katika historia ya elimu ya juu nchini Tanzania, na kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitaendelea kuzalisha wahitimu wabunifu, waadilifu, na wenye uwezo wa kuongoza nchi kuelekea uchumi wa kati na wa ngazi ya juu. “Hekima ni Uhuru,” alisema kwa msisitizo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!