Latest Posts

WA’BIASHARA WA MTWARA WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIKOPO NA MASOKO, SERIKALI YAHAKIKISHIA MABADILIKO

Wafanyabiashara wa mkoa wa Mtwara wameeleza changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku, huku wakiiomba serikali kuboresha upatikanaji wa mikopo pamoja na mazingira ya masoko, wakisema hatua hizo zitawawezesha kuongeza uzalishaji na kukuza kipato chao.

Akizungumza katika Uwanja wa Mashujaa Park, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amesema serikali imeendelea kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo ili kuwawezesha kiuchumi, lakini idadi ya wanaojitokeza kuchukua mikopo hiyo bado ni ndogo na kutoa wito kwa wafanyabiashara wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kwani fursa bado ipo na inatolewa bila vikwazo.

Mwaipaya amesema wito huo unakuja kufuatia msisitizo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuhusu dhamira ya serikali kuwawezesha wanawake na vijana kupata mitaji kwa urahisi ili waendelee kujenga uchumi wao, kwa mujibu wa Mwaipaya serikali haitarajii kuona mfanyabiashara anashindwa kupiga hatua kwa sababu tu ya kukosa mtaji.

Aidha, amewataka wanaochukua mikopo kufanya marejesho kwa wakati ili kuwapa nafasi na wengine kupata huduma hiyo kwasababu mfumo wa urejeshaji ni muhimu katika kuhakikisha mfuko wa mikopo unakuwa endelevu na unaofikia watu wengi zaidi.

Hata hivyo, Mwaipaya amewapongeza wafanyabiashara wa Mtwara kwa kuonyesha uvumilivu na juhudi katika kupambana na changamoto zinazotokea ikiwemo kupanda kwa ushuru na mabadiliko ya soko na kuongeza kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa mfano wa kuigwa kwa kutatua changamoto hizo kwa utulivu bila kufanya fujo.

Katika kueleza zaidi kuhusu mazingira ya biashara, Mwaipaya amesema serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara kuendelea kufanya shughuli zao katika Soko la Chuno, ambalo limekuwa msaada mkubwa hasa kwa wanawake wenye watoto kutokana na uwepo wa shule ndani ya eneo hilo. Aidha, soko hilo lina maeneo salama hata wakati wa mvua, jambo linalowezesha shughuli za biashara kuendelea bila usumbufu.

Kwa upande wake, mfanyabiashara Selemani Ndege amesema hatua ya kuboresha Soko la Chuno ni muhimu, lakini ameomba serikali kuzingatia maslahi ya wafanyabiashara waliopo sokoni hapo kwa kuwapa nafasi za kipaumbele katika fursa zinazotolewa na ametaja kupanda kwa ushuru kuwa moja ya changamoto inayowasumbua, na kuomba serikali kulifanyia kazi kwa makini kutokana na mkanganyiko uliopo.

Mwenyekiti wa Wamachinga mkoa wa Mtwara, Ramadhani Hassan Mtumba, amesema wamachinga wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kutopata mikopo kwa wakati, jambo linalowaathiri kwa kuwa wengi wao hawana mitaji ya kutosha na hutegemea mikopo hiyo kuendesha biashara zao hivyo ameiomba serikali kuboresha mchakato wa utoaji mikopo ili kuwasaidia wajasiriamali wadogo kusonga mbele bila kukwama,pia amesisitiza kuwa wakati wa kuboresha soko, ni muhimu kuwapangia nafasi wafanyabiashara waliopo eneo hilo badala ya kuwachukua watu kutoka maeneo mengine.

Wafanyabiashara wa Mtwara wana matumaini kwamba serikali itaendelea kuyafanyia kazi maombi na mapendekezo yao, ili kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza ushiriki wao katika uchumi wa mkoa

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!