Latest Posts

MAJIRANI WASIOPENDA KUONA TUNA AMANI NI AKINA NANI?

Na; mwandishi wetu

Oktoba 29 mwaka huu, ni siku ambayo haiwezi kusahaulika sio tu kwa Tanzania bali pia kwenye kumbukumbu za kikanda na kimataifa hasa pale wanapoiangaza Tanzania kwenye nyanja mbalimbali hususani demokrasia, haki za binadamu na utawala bora

Sio tu kwa sababu siku hiyo, Watanzania walikuwa wanafanya maamuzi ya kuchagua viongozi wanaowataka (Siku ya Uchaguzi Mkuu), lakini pia ni siku ambayo kuliibuka maandamano yaliyozaa vurugu zilizopelekea uharibifu wa mali za umma na binafsi, majeruhi, lakini kubwa kuliko yote ni kutoweka kwa watu kwenye mazingira tatanishi na vifo

Maandamano na vurugu hizo zimeripotiwa kwenye maeneo mbalimbali nchini huku mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Songwe, Njombe na Mbeya ikitajwa kuwa kinara, ambapo licha ya kushuhudiwa idadi kubwa ya waandamanaji lakini pia maafisa wa vyombo vya Ulinzi na Usalama nao wakiongozwa na Jeshi la Polisi walishuhudiwa wakijaribu kuzuia ghasia zilizojitokeza kilichofuata baada ya hapo ni historia ambayo katu si ya kukumbukwa hata kidogo,

Katika kudhihirisha ukubwa wa tatizo linalotukabili kama Taifa na kuonesha wazi kwamba tuko kwenye mtanziko unahitaji majibu ya kujuwa tunatokaje hapa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ameunda na kuzindua Tume Huru ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29 mwaka huu na siku zilizofuata, Tume inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mohamed Chande Othman

 

Wakati tukisubiri ripoti ya tume hiyo katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, na licha ya ukweli kwamba kumekuwa na maoni au mapokeo yenye mitazamo tofauti kuhusu tume hiyo, lakini bila kuingilia kazi na uhuru wa tume jambo kubwa ninalotaka kuligusia kwenye makala hii ni kuhusu kile kinachoelezwa na serikali kwamba waandamanaji walijitokeza kutokana na ushawishi kutoka nje ya nchi na wanaharakati wa mitandaoni wanaoweka ‘sumu’ inayolenga Watanzania wachome nchi yao

Hivi karibuni akiwa kwenye ziara ya kikazi Ikungi, mkoani Singida, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba alitoa wito kwa Watanzania hususani vijana kuilinda nchi, kwakuwa hata miundombinu iliyopo wanapaswa kutambua kuwa ni mali yao kwakuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa kodi zao hivyo kuiharibu ni kujirudisha nyuma wenyewe kimaendeleo

“Wengi wanaochochea haya mambo, fuatulieni, anayepaza sana sauti kuwa chomeni nchi yenu yeye hayuko hapa nchini, watoto wake hawapo hata hapa…, watu wako kwenye nchi nyingine, wanaishi kule kwingine wanawaambiaje chomeni nchi yenu?, wao watabaki na nchi yao enhee ninyi mtakuwa na ipi?, wengine kule waliko barabara yao huwezi kudondosha hata karatasi, wanaihudumia barabara yao hata karatasi hawaruhusu kutupa lakini ninyi mnaambiwa haribuni ya kwenu” -Dkt. Mwigulu

Dkt. Mwigulu alienda mbali zaidi na kueleza kuwa wengine wanaotoa ushawishi huo hasi ni majirani zetu (nchi jirani) na kwamba wanafanya hivyo kwaajili ya vita vya kiuchumi, kwakuwa wameona Tanzania inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kukuza uchumi wake kwa kasi

“Wanajuwa hawa majamaa wanataka kuwa kama Marekani hawa, wanawarundika vijana hapo, wanahamasisha vijana waliopo huku, na wale waliowarundika wengine ni Watanzania wametoa wapi hela za kuwarundika vijana wote hao nchi ya nje huko, kama hawajanunuliwa wametoa wapi hela?, Watanzania lazima tuamke, hatupendwi namna hiyo” -Dkt. Mwigulu

Sambamba na hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Gerson Msigwa akizungumza na Wanahabari Novemba 23 mwaka huu, kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam ametoa kauli zinazoshabihiana moja kwa moja na zile zilizotolewa siku chache zilizopita na Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba

Katika maelezo yake, Msigwa amewasihi Watanzania kujiepusha kushabikia na kusambaza taarifa au habari zinazochochea uhasama, hasira na kuvunja umoja wa Kitaifa, akitoa wito kwa Watanzania kung’amua mtego wa kuliangamiza Taifa, kwakuwa kwa pamoja tunapita kwenye kipindi ambacho tukiendekeza uchochezi unafanywa na watu walioko nje ya nchi, na ambao hawaguswi na chochote juu ya maisha ya Watanzania, wanaowashawishi vijana wa Kitanzania kufanya vitendo vya kuumiza nchi yetu, tutakaoangamia ni Watanzania wote

“Yaliyotokea tarehe 29 na siku kadhaa zilizofuata tulioumia ni sisi Watanzania, wanaoandika habari za uchochezi kupitia mitandao au kwenye vyombo vya habari hawapo Tanzania…, natamani Watanzania wawe wanauliza ninyi wenzetu huko mkiwa na madai mnachoma vituo vya mafuta?, mnaharibu miundombinu?, leo wananchi wa Kimara (Dar es Salaam) hawana mabasi ya kwenda katikati ya mji, mnaiba biashara za watu?, leo watu wamefirisika, watu wamejitafuta wameokota mitaj yao mnafanya hivyo?” -Msigwa

Ukichakata kwa karibu kauli hizo za serikali, utakubaliana na mimi kuwa zinaendelea kuibua maswali lukuki kuhusiana na jambo lenyewe linalotukabili, sina maana sikubalianinao la hasha, naamini serikali Ina mkono mrefu sana, na kwakuwa kauli hizo zimetolewa na viongozi waandamizi serikalini basi sina wasiwasi kabisa kuwa ni kweli kuna ‘watu wa nje’ wanataka kutuharibia nchi yetu

Lakini pamoja na mambo mengine, miongoni mwa swali la kujiuliza hapa ni hao majirani wenye roho mbaya hivyo dhidi ya nchi yetu nzuri Tanzania ni kina nani?, kwanini serikali isiamue kuwaweka hadharani kabisa?, najuwa lipo suala la kidiplomasia, lakini kama wamefikia hatua hii ni wazi kabisa wao si majirani wema kwetu, na kwakuwa hili jambo ni la Kitaifa basi ni vizuri kila mmoja wetu akamfahamu mbaya wa nchi yetu ili tujiepushe kuwa karibu

Kuna jambo nimelisikia linagusiwa na viongozi wetu wa serikali kuwa huenda baadhi ya vijana au sijuwi wote pengine walilipwa hela kufanya waliyofanya, au inawezekana hao majirani zetu wabaya ndio walilipwa hela au wanaendelea kulipwa kwaajili ya kuchoma nchi yetu, sasa hapa napo vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vinapaswa kuja na majibu iliwezekanaje mamia kwa maelfu ya watu (waliojitokeza kuandamana) wengi wao wakiwa vijana wakafikiwa, kushawishiwa hadi kufikia hatua ya dhamira yao mbaya kwa Taifa kukamilisha, au tusubiri Tume Huru ya Uchunguzi pia.

Naeleza yote haya kama tahadhari kwa serikali yangu na nchi yangu, maana lazima tujuwe kuwa Watanzania wa sasa hususani vijana ni wadadisi sana, haitoshi tu kuwaambia mambo juu juu, wanahoji sana, na wanapaswa kupatiwa majibu sahihi ili wasikubali kupokea pesa za wabaya wetu wawe upande wetu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!