Wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara wameombwa kuhuisha akaunti zao za benki ili kurahisisha mchakato wa ulipaji fedha baada ya mauzo.
Akizungumza kwenye mnada wa tatu wa zao hilo, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU, Alhaji Azam Mfaume, amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni baadhi ya wakulima kuwa na akaunti zilizolala kutokana na kutotumika kwa muda mrefu, hali inayosababisha kuchelewesha malipo yao.

Aidha, amepongeza mfumo wa kidijitali wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), akisema umeondoa changamoto nyingi zilizokuwapo enzi za mfumo wa sanduku na kuwataka wakulima kuanza kupanda mikorosho mipya kwa kutumia mbegu za kisasa na kufuata ushauri wa kitaalamu ili waendelee kunufaika na kilimo hicho, kwa kuwa mikorosho mingi waliyonayo ni ya zamani.
Ameongeza kuwa katika mnada huo wa tatu jumla ya tani 22,318,233 zimeuzwa kwa bei ya juu ya shilingi 2,700 na bei ya chini ya shilingi 2,310 kwa kilo. Aidha, katika minada miwili iliyopita, wakulima wamelipwa zaidi ya shilingi bilioni 149.
Kwa upande wake, Afisa Tarafa wa Chiungutwa, Wilaya ya Masasi, Ally Ahmed, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Masasi, amewataka wakulima kuhakikisha kuwa fedha wanazolipwa zinaonekana katika uhalisia wa maisha yao kwa kuwekeza katika elimu, ujenzi, na kutenga akiba kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake, Bakari Hassan ameishukuru Serikali kwa kuweka mifumo rafiki inayowezesha wakulima kupata bei nzuri. Hata hivyo, ameomba Serikali kuweka mfumo utakaomruhusu mkulima kupata urahisi wa kujua bei ya korosho zake ili kuepusha mkanganyiko.

“Serikali ingetengeneza mfumo ambao korosho zinapoingia ghala, mkulima ajue zipo kwenye ghala gani na lot namba ngapi, ili kupata urahisi wa kujua korosho yake imeuzwa kwa bei gani na kuondoa mkanganyiko kwa wakulima.”Amesema Bakari.