
Serikali imezitaka vyombo vya habari nchini kuhakikisha vinaelimisha jamii kuhusu umuhimu wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ili kuendeleza undugu, amani na mshikamano wa kitaifa, sambamba na kupinga upotoshaji unaoenezwa kupitia mitandao ya kijamii kwa lengo la kuleta migawanyiko.
Kauli hiyo ilitolewa Desemba 23, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamadi Yussuf Masauni, wakati akifungua Semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari iliyobeba kaulimbiu isemayo “Wajibu wa Vyombo vya Habari katika Kulinda na Kuendeleza Muungano.”
Mhe. Masauni amesema Serikali itaendelea kuulinda Muungano kwa nguvu zote, akibainisha kuwa ni mboni ya jicho la Watanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika kudumisha amani, umoja na maendeleo ya nchi.
“Muungano ni alama ya amani na maendeleo ya Taifa letu. Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuhakikisha taarifa wanazotoa ni sahihi, zina vyanzo vya kuaminika, na zinaandaa mijadala yenye tija isiyo na jazba wala kuchochea migawanyiko,” alisema Mhandisi Masauni.
Ameongeza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuangazia zaidi mafanikio ya Muungano badala ya kusubiri au kuangazia changamoto pekee.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Dkt. Festo Dugange, amesema vyombo vya habari vina jukumu muhimu la kuelimisha umma kuhusu masuala ya Muungano ili kuuhifadhi na kuufanya kuwa salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Tumeandaa semina hii mahususi kwa viongozi na wahariri wa vyombo vya habari kwa sababu ni nguzo yenye ushawishi mkubwa katika jamii,” alisema Dkt. Dugange.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi na Afya Muhimbili (MUHAS), Dkt. Harrison Mwakyembe, alisema uelewa sahihi wa historia ya Muungano ni nyenzo muhimu katika kuzuia upotoshaji unaoweza kuhatarisha mustakabali wa Taifa.
Akitoa salamu kwa niaba ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deodatus Balile, amesema vyombo vya habari vinahitaji kuimarishwa kifedha ili viweze kutoa elimu bora na endelevu kuhusu Muungano.
Ameongeza kuwa changamoto za kiuchumi zinazoikabili sekta ya habari zinaweza kudhoofisha juhudi za kuelimisha umma ipasavyo iwapo hazitashughulikiwa.