Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Athur Nanauka, amekabidhi mkopo wa vijana katika mfumo wa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 140, ambavyo vimewekewa bima.
Vifaa hivyo ni pamoja na pikipiki 15, bajaji 5 na mikokoteni ya kubebea mizigo maarufu kama “guta” 5, vitakavyowanufaisha vijana wa Mkoa wa Mtwara,ambapo hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa shilingi bilioni 200 zilizotolewa na Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi.
Ugawaji huo umefanyika leo, Machi 2, 2026, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana Mkoa wa Mtwara uliofanyika katika ukumbi wa Stella Maris Mtwara University College. Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Nanauka amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha vijana wanapata fursa za kiuchumi kupitia mikopo yenye masharti nafuu. Amefafanua kuwa vijana waliopata mkopo huo wataanza kulipa baada ya miezi mitatu, ili kuwapa nafasi ya kujiimarisha kwanza.

Aidha, ametoa wito kwa vijana kote nchini kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali kwa lengo la kujikwamua kiuchumi, pamoja na kuhakikisha wanatafuta taarifa sahihi na kuzifanyia kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, amewahimiza vijana kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika azma yake ya kuwakabidhi vijana uchumi wa nchi ,ambapo amewataka vijana wa Mtwara waliopata vifaa hivyo kuonyesha mfano bora wa matumizi sahihi ya mikopo ili wengine pia waweze kunufaika.
Naye Katibu wa Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Mtwara, Hashimu Ally, amesema uamuzi wa serikali kutoa mikopo kwa mfumo wa vifaa badala ya fedha taslimu ni hatua nzuri, kwani awali baadhi ya vijana hawakuwa na uelewa wa namna bora ya kutumia fedha walizokopa. Ameeleza kuwa mfumo huo utasaidia kulinda mtaji wa vijana, kwa kuwa vifaa walivyokabidhiwa ndivyo vitakavyowaingizia kipato.
