Mjadala wa kitaifa kuhusu mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya nchini Tanzania umeingia katika hatua mpya na kuibua hisia mseto miongoni mwa wanasiasa, wasomi, mashirika ya kiraia na wananchi wa kawaida, kutokana na mfululizo wa kauli zilizotolewa na viongozi wa juu wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mchakato huo ambao umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu na pande zote za kisiasa, umeshika kasi zaidi kutokana na hotuba iliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, tarehe 24 Julai, 2026. Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Dkt. Nchimbi alitoa wito wa wazi na wa kimkakati akiwataka Watanzania kutolala wala kurudi nyuma katika harakati za kudai Katiba Mpya.
“Nikiambiwa kuna jambo tu kama Makamu wa Rais waambie watanzania, nitasema pambaneni mpate katiba mpya, katiba ambayo ina makubaliano ya wadau wote, katiba yenye muafaka katika taifa, katiba ambayo kila Mtanzania popote alipo atajiskia fahari kujitambulisha mimi natoka Tanzania, katiba inayojali maisha”, alisema Dkt. Nchimbi.
Katika ufafanuzi wake, Dkt. Nchimbi alieleza kuwa nia na utashi wa Rais aliyeko madarakani ni nguzo kuu katika kukamilisha mchakato huo. Alibainisha kuwa Katiba ya sasa inampa Rais mamlaka makubwa mno, na kwamba pasipo utashi wa dhati kutoka kwa Mkuu wa Nchi, mchakato wa Katiba unaweza kukwama kwa miaka mingi. Dkt. Nchimbi alisisitiza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ana utashi na nia thabiti ya kuruhusu mchakato huo utekelezwe.
Hata hivyo, saa chache tu baada ya hotuba hiyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, Mohamed Kawaida alichapisha ujumbe kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram ambao umetafsiriwa kuwa jibu la kuzuia kile kilichotafsiriwa kama ukiukaji wa nidhamu ya chama na wafuasi wake kwenye ukurasa huo na wachambuzi wa siasa, na jibu kwa Dkt. Nchimbi.
Andiko hilo liliambatana na kipande cha video kikimwonesha Prof. Kitila Mkumbo, alipokuwa akieleza wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM jijini Dodoma Mei 30, 2025 kuwa ajenda ya Katiba Mpya ni ahadi rasmi na ya kisera ya CCM. Prof. Kitila ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025- 2030 alibainisha kuwa mchakato huo tayari umeingizwa kwenye Ilani hiyo na kwamba Serikali inatenda kazi chini ya maelekezo hayo ya chama.
Katika ujumbe wake, Mohamed Kawaida alikazia umuhimu wa taasisi kusimamia misingi yake na kuzuia hali ya viongozi kujitengenezea umaarufu binafsi kupitia ajenda za chama.
“Chama cha siasa ni taasisi inayojengwa juu ya misingi ya utaratibu wa ndani, uwajibikaji wa pamoja, nidhamu ya chama, na uongozi wa pamoja. Uimara wa taasisi haupimwi kwa umaarufu wa mtu mmoja isipokuwa kwa uwezo wake wa kulinda taratibu, utamaduni na maamuzi ya pamoja. Pale ambapo viongozi au makada huanza kutanguliza malengo binafsi kuliko maamuzi ya taasisi hujitokeza kile kinachoitwa ‘personalisation of power’…hali ambayo maslahi ya mtu binafsi hupewa uzito kuliko uhalali wa taasisi”, ameandika Kawaida.
Kawaida ameongeza kuwa, kwa mtazamo wa kiongozi wa taasisi, michakato ya kumpima au kumchambua kiongozi si adhabu bali ni sehemu ya uwajibikaji wa kitaasisi na utawala bora wa ndani. Amehitimisha kwa kusema kuwa taasisi imara hudumu milele wakati viongozi ni watu wa kupita, na kwamba CCM itaendelea kuongozwa na utamaduni wake wa nidhamu na uwajibikaji wa pamoja kuliko matakwa ya mtu mmoja.
“Hatimaye, wanaoendana na maadili na misingi ya taasisi huendelea kubeba dhamana ya uongozi huku wale wanaotanguliza maslahi binafsi wakijitenga wenyewe na misingi waliyopewa kuisimamia. Kwa msingi huo uimara wa chama hauko katika uwezo wa kiongozi mmoja kujijengea taswira mbele ya umma bali katika uwezo wa taasisi kusimamia nidhamu, kulinda maamuzi yake ya pamoja na kuhakikisha kuwa uongozi unabaki kuwa wa taasisi badala ya kuwa wa mtu mmoja”, ameeleza Kawaida.
Mjadala huu unakuja kukiwa na muendelezo wa kauli kutoka kwa viongozi wengine wa CCM kuhusu Katiba Mpya. Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Ally Hapi, alipokuwa akizungumza mkoani Shinyanga, alitoa wito kwa Watanzania kutokubali ajenda ya Katiba Mpya ihodhiwe na vyama vya upinzani kama CHADEMA. Hapi alieleza kuwa Katiba Mpya ni takwa pana la kitaifa linalohusu maslahi ya wananchi wote, na kwamba CCM imeshaweka mwelekeo wa wazi wa namna ya kuitekeleza kupitia serikali yake. Naye, Prof. Mkumbo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CCM) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji akizungumza hivi karibuni bungeni jijini Dodoma alieleza kuwa ajenda ya Katiba Mpya ni ‘mali ya CCM’ kwa kuwa tayari imeingizwa rasmi katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 katika kile kilichoelezwa pia kama jibu kwa vyama vya upinzani ambavyo vilikuwa vikieleza kuhusu kuharakisha mchakato wa katiba mpya kupitia yao mikutano mbalimbali ya hadhara.