Tanzania na Oman zimeingia katika hatua mpya ya ushirikiano wa sekta ya habari baada ya kusainiwa kwa Mikataba ya Ushirikiano (MoU) kati ya Chama cha Waandishi wa Habari wa Oman (OJA) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), pamoja na Chama cha Wafanyakazi Katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), kwa lengo la kuimarisha taaluma, kubadilishana uzoefu na kufungua fursa za kiuchumi.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo Alhamisi, Oktoba Mosi, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa kongamano la ushirikiano baina ya wanahabari wa Tanzania na Oman lililowakutanisha waandishi wa habari kutoka nchi hizo mbili.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Abdallah Kilima, amesema kongamano hilo limefungua ukurasa mpya katika ushirikiano wa Tanzania na Oman ambao umejengwa kwa misingi ya historia, utamaduni, biashara na undugu wa muda mrefu.
Balozi Kilima amesema wanahabari wana nafasi muhimu katika kuwajengea vijana uelewa sahihi kuhusu historia ya mahusiano ya nchi hizo mbili, akieleza kuwa matukio ya michezo kama Kombe la Ghuba na AFCON yanaweza kutumika katika kubadilishana tamaduni na kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania na Oman.
Ameongeza kwa kusema kuwa, ushirikiano huo pia utajikita katika mafunzo ya habari za kidijitali, uhakiki wa taarifa na matumizi ya kiwajibikaji ya Akili Unde (AI), huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na mpango kazi wa miezi 12 wa kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo.
Kwa upande wake, Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud Bin Hilal Bin Saud Al Shidani, amesema uhusiano wa Tanzania na Oman una misingi imara ya kihistoria, huku matumizi ya Kiswahili, Kiarabu na Kiingereza yakirahisisha mawasiliano na ushirikiano kati ya wananchi wa nchi hizo.
Amesema zaidi ya waandishi wa habari 50 kutoka Oman wamefika Tanzania kwa ajili ya kushiriki kongamano hilo, ambalo litasaidia kujenga uwezo, kubadilishana maarifa na kuimarisha maadili ya uandishi wa habari katika kipindi cha ukuaji wa mitandao ya kijamii.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Oman (OJA) , Dkt. Mohamed bin Mubarak Al Araimi, amesema ushirikiano wa Oman na Tanzania una mizizi mirefu ya kitamaduni na kijamii, huku Zanzibar ikiwa sehemu muhimu ya historia ya mahusiano hayo.
Amesema habari haina mipaka na inaweza kuwa daraja linalounganisha watu na mataifa, hivyo kuwataka wanahabari kutumia kalamu zao kuhifadhi historia na kusimulia habari za kweli zinazojenga uhusiano kati ya Tanzania na Oman.
Dkt. Al Araimi ameendelea kwa kusema kuwa, kongamano hilo pia limefungua fursa za ushirikiano katika sekta za habari, utalii, uchumi na uwekezaji, akitaja pia mchango wa magazeti ya kihistoria ya Zanzibar, yakiwemo Al-Falaq na Al-Najah.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema matumizi ya Kiswahili katika kongamano hilo yanaonesha fahari ya lugha hiyo na umuhimu wake katika kujenga uhusiano kati ya jamii za Tanzania na Oman.
Balile amesema TEF ina dhamira ya kuimarisha uweledi, uhuru wa uhariri, uendelevu wa vyombo vya habari na uwajibikaji kwa jamii, huku akisisitiza kuwa magazeti bado yana nafasi katika kutoa habari sahihi licha ya kukua kwa mitandao ya kijamii.
Ameunga mkono kuwepo kwa mpango kazi wa miezi 12 na kupendekeza kuwe na waratibu wawili au watatu watakaosimamia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Musa Juma Siwayombe, amesema kongamano hilo ni hatua mpya kwa sababu linawashirikisha moja kwa moja wanahabari katika kuendeleza mahusiano ya Tanzania na Oman.
Siwayombe amesema kongamano hilo linajadili masuala ya uhuru wa habari, kubadilishana uzoefu wa kiteknolojia na fursa za uwekezaji, akiwataka wawekezaji kutoka Oman kuangalia fursa za kuwekeza katika sekta ya habari nchini Tanzania, ikiwemo televisheni, redio na magazeti.
Amesema uwekezaji huo unaweza kuchangia ukuaji wa uchumi wa vyombo vya habari na kuboresha mazingira ya kazi kwa wanahabari, huku akiwakaribisha wageni kutoka Oman kama sehemu ya familia ya Tanzania.
