
Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu Novemba Mosi, 2026 imefanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa mabirika ya kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Sanga Sanga, Kitongoji cha Masanza, Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.
Mradi huo umefikia asilimia 45 ya utekelezaji na unatarajiwa kuhudumia kaya 31 pamoja na mifugo 1,234 wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo katika vitongoji vya Masanza na Rubungo.
Mradi huo unalenga kuboresha uhifadhi wa mazingira na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo, pamoja na kurahisisha shughuli za ufugaji kwa wananchi wa maeneo hayo ili kuacha tabia ya kupeleka mifugo moja kwa moja kwenye vyanzo vya maji.
Katika hatua nyingine, wataalamu wamekagua eneo la ujenzi wa banio (Check dam) katika Mto Ngerengere ambapo mradi huo mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 100.
Mradi huo wa banio utasaidia kudhibiti mmomonyoko wa udongo na kupunguza kiasi cha mchanga na tope linalosafirishwa na maji na kupelekwa kwenye Bwawa la Mindu.