Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Shadrack Nyaulingo, amewataka wahitimu wa Umoja wa Makanisa yenye Huduma ya Mtoto na Kijana wanaoshirikiana na Compassion International Tanzania kuwa chachu ya kuwasaidia watu wenye uhitaji, ikiwa ni njia ya kurejesha fadhila kwa jamii iliyowasaidia.
Nyaulingo ameyasema hayo, katika Mahafali ya Pili ya wahitimu hao, alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo.

Amesisitiza kuwa wahitimu wanapaswa kutambua kusudi la maisha yao na kutumia elimu, maarifa na vipaji walivyovipata kwa ufanisi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Aidha, ameishukuru Compassion International Tanzania pamoja na walezi kwa uwekezaji wao katika maisha ya watoto na vijana hao, akieleza kuwa juhudi hizo zina matarajio ya kuizalishia jamii madaktari na wataalamu mbalimbali siku zijazo.

Kwa upande wao, wahitimu hao wameiomba Serikali, jamii na wadau mbalimbali kuongeza fursa za ajira zitakazowawezesha kujitegemea kiuchumi na kuendesha maisha yao baada ya kuhitimu.
Wakizungumza kupitia risala yao iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi, wamesema huduma hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa watoto na vijana wanaoishi katika mazingira magumu, huku ikiwafikia zaidi ya vijana 200.

Vilevile, wameiomba Serikali kuwawezesha kupata elimu kuhusu mikopo inayotolewa na Serikali ili waweze kufahamu taratibu na fursa zilizopo kwa ajili ya kuanzisha shughuli za kujipatia kipato.
Aidha, wameomba kuongezewa mafunzo na ujuzi katika maeneo mbalimbali ili kuimarisha uwezo wao na kuwawezesha kukabiliana na changamoto za soko la ajira, huku wakitumia elimu waliyoipata kujenga maisha bora na kuchangia maendeleo ya jamii.
