Latest Posts

DC LUGANGIRA AKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA UPINZANI, ASISITIZA UTEKELEZAJI WA 4R ZA RAIS SAMIA

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Bi. Neema Lugangira, amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa vyama vya upinzani katika ofisi yake, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha maridhiano, ushirikiano na mshikamano wa kisiasa kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Mazungumzo hayo ni sehemu ya hatua za awali za Lugangira katika kutekeleza majukumu yake wilayani Arumeru, kwa kuzingatia misingi ya 4R iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayojumuisha maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya.

Lugangira amesisitiza umuhimu wa Serikali na vyama vya siasa kuendeleza mawasiliano na ushirikiano katika kutatua changamoto za wananchi, kudumisha amani na kuhakikisha kuwa tofauti za kiitikadi haziwi kikwazo katika kuleta maendeleo.

Ameeleza kuwa dhamira yake ni kushirikiana na wadau wote, bila kujali tofauti za vyama vya siasa, ili kuhakikisha wananchi wa Arumeru wanapata huduma bora na fursa za maendeleo kwani hayo ndio maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa Arumeru Mashariki, Pallangyo Penzila, amempongeza Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuanza kwa kujifunza na kuifahamu wilaya pamoja na wananchi wake kabla ya kuendeleza majukumu yake.

Penzila amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kiongozi anayeanza majukumu katika eneo jipya, akieleza kuwa kulifahamu eneo na watu wake ni msingi wa kufanya maamuzi sahihi na kuleta maendeleo. Ameongeza kuwa elimu, uzoefu na wito wa Lugangira katika utumishi wa umma vinaweza kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Meru iwapo kutakuwa na ushirikiano wa dhati bila kujali tofauti za kisiasa.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP) kwa upande wa Arumeru Mashariki, Bi.Magdalena Masaka, amemshukuru Lugangira kwa kuanza majukumu yake kwa kukutana na wawakilishi wa vyama vya siasa, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha utayari wa kujenga ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa kisiasa.

Masaka amesema vyama vya siasa havipo kwa ajili ya uchaguzi pekee, bali pia vina jukumu la kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo, kulinda amani na kudumisha utulivu katika maeneo yao.

Ameeleza kuwa wao kama vyama vya upinzani wako tayari kuendelea kushirikiana na Mkuu wa Wilaya pamoja na Serikali kwa ujumla katika kuhakikisha wananchi wa Arumeru wananufaika na juhudi za maendeleo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!