Jeshi la Magereza Tanzania limesisitiza kuwa mawakili wanaomwakilisha Mahabusu Tundu Lissu wanaendelea kuruhusiwa kuonana na mteja wao gerezani kwa mujibu wa sheria mara baada ya kujiridhisha kuwa ni mawakili wake halali, likikanusha madai ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa mawakili wa kiongozi huyo wamekuwa wakizuiwa kuingia gerezani.
Akiwasilisha taarifa rasmi kwa umma leo, Oktoba 27, 2026, Msemaji wa Jeshi la Magereza, SACP Elizabeth Mbezi amefafanua kuwa taarifa zinazosambazwa na CHADEMA kuhusu kuzuiwa kwa mawakili si za kweli na zinalenga kuleta taharuki katika jamii.
“Kuhusu kutembelewa na mawakili wanaomwakilisha wameendelea kuruhusiwa kuonana na mteja wao kwa mujibu wa taratibu baada ya kujiridhisha kuwa ni mawakili wake na si vinginevyo. Jambo hili limekuwa likitekelezwa kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zilizopo”, ameeleza SACP Mbezi.
SACP Mbezi ameongeza kuwa Jeshi la Magereza linazingatia sheria, utu na misingi ya haki za binadamu katika kuwahifadhi mahabusu wote, huku akibainisha kuwa Mwenyekiti huyo wa CHADEMA yupo salama na wala hayupo kwenye mgomo wa kula kama ilivyodaiwa.
Ufafanuzi huo wa Jeshi la Magereza unakuja kufuatia taarifa iliyotolewa tarehe 26 Oktoba 2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, aliyedai kuwa mawakili watatu wa Tundu Lissu walizuiwa kuingia gerezani kumuona mteja wao.
Kwa mujibu wa Rupia, mawakili hao, Dickson Matata, Doris Kafuku, na Neema Massame walifika gerezani tarehe 26 Oktoba 2026 kwa lengo la kumtembelea na kuwasiliana na Lissu, lakini walizuiwa kuingia ndani na mamlaka za gereza hilo, jambo linalohatarisha haki yake ya msingi ya kupata msaada wa kisheria.