Latest Posts

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YARATIBU UPIMAJI MACHO KWA WATUMISHI, YASISITIZA AFYA NI MTAJI

 

 

WIZARA ya Maliasili na Utalii, kupitia Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, imeratibu zoezi la upimaji wa macho kwa watumishi wake katika ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma, ili waweze kufanya uchunguzi na kuchukua hatua madhubuti za kutibu afya zao mapema, huku ikisisitiza kuwa afya ya mtumishi wa umma ni mtaji kwa mwajiri na huboresha utendaji kazi mahali pa kazi.

Akizungumzia zoezi hilo, Afisa Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Getrude Kassara, amesema upimaji huo unawawezesha watumishi kuchukua hatua za mapema za kutibu afya zao.

Ameongeza kuwa afya ya mtumishi wa umma ni mtaji kwa mwajiri, hivyo upimaji huo utasaidia utendaji kazi mahali pa kazi, ikizingatiwa kuwa vifaa vingi vinavyotumika ni vile vinavyoweza kuathiri macho kwa namna moja au nyingine.

“Idara ya Utawala a Usimamizi wa Rasilimali Watu imeona ni vyema kuisogeza huduma hii kwa watumishi wetu, ambao mara nyingi wanakuwa na majukumu mengi, hivyo kupitia kampuni ya Kliniki Right Cycles Opticals tumeweza kutekeleza hilo,” alisema Kassara.

Kwa upande wake, Diana Vainga kutoka Idara ya Misitu na Nyuki amesema huduma ya upimaji macho iliyotolewa leo na kuratibiwa na Sehemu ya Rasilimali Watu imekuwa na manufaa kwake na kwa watumishi wengine.

Amesema huduma hiyo imemsaidia kupata matibabu ya macho, kwani awali alikuwa akisumbuliwa na tatizo hilo.

Naye Daniel Coernel kutoka Wizara hiyo ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watumishi wengine kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara.

Aidha, ametoa pongezi kwa Wizara kwa hatua iliyochukua ya kuhakikisha watumishi wanapima afya.

Zoezi hilo limehudhuriwa na watumishi mbalimbali, wakiwemo Wakurugenzi wa Idara na Vitengo pamoja na wafanyakazi kutoka katika Idara na Vitengo hivyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!