Latest Posts

“VTS NI YA MUDA, TUNAENDA KWENYE MFUMO KAMA VAR”: KATAMBI AAHIDI TEKNOLOJIA MPYA NA MWISHO WA UONEVU BARABARANI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi ametangaza hatua za Serikali kutatua kero za Mfumo wa Kufuatilia Magari (VTS) pamoja na kupiga marufuku vitendo vya askari wa usalama barabarani kufanya kazi kwa kuviziana na kutegana.

Katika mkutano huo uliofanyika kufuatia mgomo wa madereva uliodumu kwa siku mbili tangu tarehe 29 Septemba 2026, Katambi alikiri kuwepo kwa migongano ya kitakwimu kati ya kamera za usalama barabarani na mfumo wa VTS. Alibainisha kuwa zipo maeneo ambapo kamera ya trafiki inasoma spidi 100 huku VTS ikionyesha spidi 130, hali inayowasababishia madereva kero zisizokuwa za lazima.

Akitangaza hatua ya kiserikali kufuatia maelekezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Katambi alisema:

“Zipo ambazo zimekuwa na changamoto na ukiangalia kuna maeneo kamera ya trafik imesoma spidi 100 VTS inasoma 130… kwa hiyo hizi changamoto kwa maelekezo ambayo tumeyapata pia kwa ofisi ya waziri mkuu tunakwenda kukaa wizara ya ujenzi, wizara ya uchukuzi, wizara ya mambo ya ndani ya nchi lakini pia wizara ya kazi, ajira na mahusiano ili kwenda kulichakata jambo hili na kuweka utaratibu mzuri zaidi.”

Katambi alieleza kuwa mfumo wa VTS ni wa muda katika kipindi hiki cha mpito, akiorodhesha jinsi Serikali ilivyowahi kuondoa mfumo wa ‘gavana’ ulipojenga changamoto hapo awali.

Alisema nchi inaelekea kwenye teknolojia ya kisasa ya udhibiti wa spidi barabarani inayofanana na mfumo wa VAR kwenye mpira wa miguu, ambapo kamera za kisasa zitafungwa barabarani na kurekodi makosa moja kwa moja bila kudhibitiwa na askari, ili kuzuia uonevu au upendeleo.

Katika hatua nyingine, Katambi alipiga marufuku utaratibu wa baadhi ya askari au watu wasio waaminifu kufanya kazi kwa kuviziana, kutegana au kuendesha magari taratibu mbele ya madereva ili kuwanasa na kuwapiga faini

Akiweka msisitizo kuhusu marufuku hiyo, Waziri Katambi alisema: “Mlizungumzia kuhusiana na uonevu, ubabe na vitu kama hivyo lakini pia kufanya kazi kwa kuviziana na kutegana… leo nasema hatutafanya kazi kwa kuviziana na kutegana, ule utaratibu ni marufuku… sio mtu unategesha gari pale unaendesha kwa spidi ndogo ili kumkamata dereva… tumekubaliana na jeshi la polisi, IGP ametoa maagizo na maelekezo mahususi ya utekelezaji wa jambo hili.”

Aliongeza kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) amemwekea maelekezo Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani (Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mkonda) pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha marufuku hiyo inasimamiwa na kutekelezwa kikamilifu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!