Latest Posts

UONGEZAJI THAMANI MADINI AJENDA KUU MKUTANO WA MADINI 2026

Tanzania inatarajiwa kuwa Kitovu cha Majadiliano ya kimataifa kuhusu uwekezaji katika Sekta ya Madini, huku wadau 1,715 kutoka ndani na nje ya nchi wakitarajiwa kushiriki Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC 2026), unaolenga kuimarisha uwekezaji, kukuza viwanda na kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini pamoja na kuhamasisha uongezaji thamani madini ndani ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam Novemba 17, 2026, Waziri wa Madini,  Mhe. Anthony Mavunde, amesema mkutano huo utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, mwaka huu na kufunguliwa na Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan,  utawakutanisha wadau mbalimbali kujadili fursa za uwekezaji na maendeleo ya Sekta ya Madini.

Mhe. Mavunde amesema hadi leo Novemba 17, mwaka huu, washiriki 1,715 wamethibitisha kushiriki mkutano huo, wakiwemo 226 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Amesema  washiriki wengine ni Mawaziri wa Madini kutoka nchi mbalimbali, viongozi wa kampuni za kimataifa, taasisi za fedha, watafiti, mabalozi, wachimbaji wadogo, wafanyabiashara wa madini, waongezaji thamani na watoa huduma migodini.

Alizitaja nchi ambazo Mawaziri wa Madini wanatarajiwa kushiriki kuwa ni Afghanistan, Kenya, Uganda, Mali, Ghana,  Rwanda, Burundi, Saudi Arabia na Somalia.

Mhe. Mavunde amesema mkutano huo utakuwa na watoa mada zaidi ya 57 kutoka Afrika, Ulaya, Asia, Mashariki ya Mbali na Marekani, watakaobadilishana uzoefu na kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya madini, hususan uongezaji thamani.

Amesema kaulimbiu ya mkutano huo ni ‘Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi’ inayolenga kuhamasisha matumizi ya rasilimali za madini katika kukuza uchumi wa viwanda, kuongeza ajira na kuhakikisha rasilimali hizo zinanufaisha zaidi Taifa.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mkutano huo utatoa fursa za kuvutia uwekezaji, kutangaza utajiri wa madini wa Tanzania, kuimarisha masoko ya madini nje ya nchi, kukuza ushirikiano wa kibiashara na kuhamasisha matumizi ya teknolojia na utaalamu katika shughuli za uchimbaji na uchakataji.

Aliongeza kuwa mkutano huo utaambatana na vikao vya pembeni vya Mawaziri wa Madini, mikutano ya kibiashara kati ya kampuni na kampuni (Business to Business), Kituo cha Pamoja cha Serikali (Government One Stop Centre), mafunzo ya uongezaji thamani madini (Master Class) na maonesho ya madini.

Pia, kutakuwa na hafla ya Usiku wa Madini itakayohusisha utoaji wa tuzo kwa wadau waliofanya vizuri katika makundi mbalimbali.

Aidha, akizungumzia mafanikio Waziri Mavunde amesena  katazo la kusafirisha madini ghafi nje ya nchi imesaidia kuongeza viwanda vya ongezaji thamani madini ambapo katika sekta mchango katika Pato la Taifa umeongezeka hadi asilimia 10.3 mwaka 2025 kutoka asilimia 7.8 mwaka 2024.

“Mpaka sasa tuna viwanda vya kusafisha dhahabu nane, viwanda 16 vinajengwa vya uongezaji thamani madini ya shaba, Dodoma pekee kuna viwanda tisa,” amesema Waziri Mavunde

Pia, amesema pia Kilwa kimezinduliwa kiwanda kikubwa cha madini chumvi chini ya STAMICO wakati Songwe kinajengwa kiwanda kikubwa cha nne duniabi cha kuchakatw madini hadimu ya Niobium.

Amesema thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi nayo imeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 4.12 mwaka 2024 hadi Dola bilioni 5.40 mwaka 2025.

Katika upande wa mapato ya Serikali, amesema makusanyo yatokanayo na sekta ya madini yameongezeka kutoka Sh bilioni 526 katika mwaka wa fedha 2020/2021 hadi Sh trilioni 1.39 katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Aidha, amesema ununuzi wa bidhaa na huduma katika sekta hiyo umeongezeka kutoka Sh bilioni 884.09 mwaka 2010 hadi Sh trilioni 5.2 mwaka 2025, hali inayotokana na usimamizi wa Sera ya Ushirikishwaji wa Wazawa.

Amesema pia, ajira rasmi katika sekta ya madini zilifikia 19,874 hadi Aprili 2025, ambapo asilimia 97.4 ya ajira hizo zilikuwa za Watanzania.

Kuhusu wachimbaji wadogo, Mavunde amesema mchango wao umefikia takribani asilimia 40 ya uzalishaji wa madini nchini, kutokana na hatua za Serikali za kuimarisha masoko ya madini, vituo vya ununuzi na upatikanaji wa vifaa, teknolojia na mitaji.

Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuwezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo kupitia mabenki na taarifa za kijiosayansi zitakazosaidia shughuli zao.

Katika hatua nyingine, alisema kwa mara ya kwanza Tanzania imefanikiwa kutunga sheria inayotenga asilimia 10 ya mapato ya kila mwaka yatokanayo na sekta ya madini kwa ajili ya kufadhili shughuli za utafiti wa madini.

Pia, Serikali imesaini mikataba ya makubaliano ya mfumo wa uwekezaji (Mining Framework Agreements) na kampuni 14 za ubia kwa ajili ya kuendeleza miradi ya madini ya kinywee, nikeli, niobium, madini adimu ya ardhini (REE) na gesi ya helium.

Mavunde alitoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia sekta ya madini na kuweka mazingira yanayowezesha ukuaji wa uwekezaji, akisema mafanikio yaliyopatikana yametokana na jitihada za Serikali katika kuboresha usimamizi wa rasilimali, kuongeza mapato na kupanua ushiriki wa Watanzania.

Katika mkutano huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuufunga Novemba 21, huku Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya Usiku wa Madini.

Waziri huyo amewakaribisha wadau wa sekta ya madini kutoka ndani na nje ya nchi kushiriki mkutano huo, akisisitiza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kuitangaza sekta ya madini na kuvutia wawekezaji nchini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!