Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza, amedai kupokea vitisho vya yeye kupotezwa au kuuawa kufuatia andiko lake la hivi karibuni lililopewa jina la “Naanika ujinga wangu na kuficha hekima yangu”, huku akisisitiza kuwa safari hii anaamini wanaomtishia “hawatanii”.
Akizungumza tarehe 16 Novemba 2026 kwenye mahojiano maalum na Wino Tanzania, Askofu Bagonza ameeleza kuwa vitisho vya aina hiyo si mara ya kwanza kuvipata, lakini kwa mara hii anaona viashiria vya dhahiri vinavyoonesha kuwa waliotuma vitisho hivyo wana nia ya dhati ya kutekeleza azma yao.
Askofu Bagonza ameeleza kuwa vitisho na shinikizo analopitia vinatoa taswira kwamba mamlaka za nchi na uongozi wa kitaifa unahujumiwa kutoka ndani ya mfumo wenyewe na watu wenye nia mbili. Amebainisha kuwa haiwezekani raia wa kawaida aliye na mahangaiko ya maisha akatishia uhai wa mtu aliyetoa maoni yake, bali watu walio ndani ya mfumo ndio wanaofanya matendo hayo na kumchonganisha Mkuu wa Nchi na wananchi.
“Hawaniingilii au hawanihujumu mimi, wanamhujumu yule wanayemtetea. Nahisi mamlaka zimechelewa kugundua kwamba kuna wahujumu ndani ya mfumo”, ameeleza.
Kiongozi huyo wa kiroho ameeleza kushangazwa na jinsi baadhi ya watu wanavyokimbilia kumshambulia binafsi na kuanza kumvua uraia wake kwa kumwita ‘Mnyarwanda’ anayeishi Karagwe, badala ya kujibu hoja na mawazo anayoyaweka wazi kwenye maandiko yake.
“Kwahiyo ninaamini hawatanii, hawatanii lakini tatizo ni kwamba nilichokiandika ni ujinga wangu. Kwanini wasije na hekima yao inayopingana na ujinga wangu?”, amehoji Askofu Bagonza.
Ametahadharisha kuwa hatua ya kubana uhuru wa kujieleza na kutishia wanaotoa maoni inaleta athari kubwa kwa demokrasia, kwani inasababisha wananchi kuichukia serikali na kufanya upinzani usibaki tena kwa vyama vya siasa kama CHADEMA, bali uhamie moja kwa moja mioyoni mwa wananchi wote wanaopokwa uhuru wao.
Pamoja na kuwepo kwa vitisho hivyo, Askofu Bagonza amesisitiza kuwa hana hofu na yuko tayari kwa lolote linaloweza kutokea.