Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amemtaka kiongozi yeyote wa dinimwingine anayedai kupokea vitisho vya kuuawa au kupotezwa, kwenda kutoa taarifa rasmi katika Jeshi la Polisi badala ya kuandika au kulalamika kwenye mitandao ya kijamii
Akizungumza leo katika mahojiano maalum ndani ya kipindi cha Kasri kinachorushwa na Crown FM, Msigwa amebainisha kuwa utaratibu wa kukimbilia mitandaoni badala ya kutoa taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama unakwamisha juhudi za kuwabaini na kuwakamata waliohusika na vitisho hivyo.
Kauli ya Msemaji Mkuu wa Serikali inajiri saa chache baada ya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza kudai kuwa amepokea vitisho vya kupotezwa au kuuawa kufuatia andiko lake lililopewa jina la “Naanika ujinga wangu na kuficha hekima yangu”.

Hata hivyo, Msigwa amesisitiza kuwa njia sahihi na ya kiusalama kwa mtu yeyote anayepokea kitisho ni kuwasilisha ushahidi na taarifa kamili kwa Jeshi la Polisi ili vyombo vya dola viweze kuchukua hatua za kisheria.
Ameongeza kuwa kutangaza kutishiwa kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kabla ya kuripoti polisi kunawapa mwanya watuhumiwa waliotoa vitisho hivyo kujificha au kufuta ushahidi
“Wewe unapata kitisho unakwenda kwenye mtandao wa kijamii unazungumza, hivi hao walikutisha si ndio wanapotea? Kwa nini usiende kwenye chombo cha ulinzi na usalama uambie nimepokea kitisho kama ni kwenye simu kutoka kwenye simu hii ama kutoka kwenye jukwaa hili ama kutoka kwa fulani ili vyombo vya ulinzi na usalama vichukue hatua,” alieleza Msigwa