Latest Posts

ACAF YAMWANDIKIA RAIS SAMIA KUHUSU KUKAMATWA KWA WAHADHIRI , “WAACHIWE”

Shirika la Kikanda la Uhifadhi wa Uhuru wa Taaluma Afrika (Africa Coalition for Academic Freedom – ACAF) limemwandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, likieleza wasiwasi wake kuhusu kuendelea kushikiliwa kwa wahadhiri watatu wa vyuo vikuu waliokamatwa mapema mwezi Julai 2026.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Kanda wa ACAF, Profesa Kwadwo Appiagyei-Atua, shirika hilo limewataja wahadhiri hao kuwa ni Johaiven Revelian Bikongolo na Titus Joseph Kituli kutoka Chuo Kikuu cha St. John’s Tanzania (SJUT), pamoja na Melkisedeki Kaijage wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

ACAF imeeleza kuwa kukamatwa kwao kunazua hofu kuhusu hali ya uhuru wa taaluma na kujieleza nchini, kutokana na taarifa kuwa walikamatwa kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano ya Julai 7, 2026. Shirika hilo limesikitishwa zaidi na taarifa kuwa mmoja wa wahadhiri hao alikamatwa baada ya kufundisha somo la Maadili na Utawala Bora kwa kutumia mifano ya kashfa za kihistoria za ufisadi nchini kuelezea uwajibikaji hatua inayoweza kutafsiriwa kama adhabu dhidi ya ufundishaji na mijadala halali ya kitaaluma.

Aidha, ACAF imeeleza wasiwasi wake kuwa miongoni mwa wahadhiri hao wameendelea kushikiliwa kwa zaidi ya siku 17 bila kufikishwa mahakamani wala kupewa dhamana, huku familia na waajiri wao wakidaiwa kutoarifiwa kwa wakati, jambo linalokwenda kinyume cha utawala wa sheria.

“Vyuo vikuu vipo kwa ajili ya kuchochea fikra pevu, mijadala yenye ushahidi, na ubadilishanaji huru wa mawazo. Wanataaluma lazima waweze kufundisha, kufanya tafiti, na kushiriki katika mijadala ya umma bila hofu ya kutishwa, kukamatwa, au kuingiliwa kisiasa. Kugeuza mijadala ya darasani au uchambuzi wa kisomi kuwa makosa ya jinai hakudhoofishi tu uhuru wa taaluma, bali pia mfumo wa elimu ya juu na utawala wa kidemokrasia,” imeeleza taarifa hiyo ya ACAF.

Kutokana na hali hiyo, ACAF imeiomba Serikali kuwaachia huru mara moja na bila masharti wahadhiri hao, isipokuwa kama kuna mashtaka ya jinai yenye ushahidi yatakayowasilishwa mahakamani kwa haraka. Pia imetaka kuheshimiwa kwa haki zao za kisheria na kulindwa kwa uhuru wa taasisi za elimu ya juu kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na mikataba ya kimataifa.

Barua hiyo ya ACAF pia imenakiliwa kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Dkt. Paul Loisulie, mmoja wa wahadhiri wa SJUT alikamatwa kufuatia mada hiyo ya utawala bora (akitumia mifano kama Richmond na Escrow), huku mwingine ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi akihusishwa na masuala ya uchaguzi wa wanafunzi chuoni hapo.

Wakati huohuo, Mhadhiri wa UDOM, Melkisedeki Kaijage, alibadilishiwa mashtaka yake kuwa ya ugaidi kutoka uchochezi. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma UDOM (UDOMASA), Dkt. Gerald Shija, alithibitisha kuwa Kaijage ambaye amekuwa mikononi mwa polisi tangu Julai 8, 2026 alikuwa katika mchakato wa kukamilisha vigezo vya dhamana vilivyotolewa na Mahakama tarehe 21 Julai, kabla ya hati yake ya mashtaka kubadilishwa na kusomewa mashtaka hayo mapya ya ugaidi ambayo hayana dhamana.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!