Latest Posts

MWIPOPO AWASIHI WANAWAKE CCM KUGOMBEA UONGOZI, ATOA MIL. 4/- KUSAIDIA DENI LA VIWANJA

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Dickson Mwipopo, amewataka wanawake ndani ya chama hicho kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, akisisitiza kuwa ujenzi na maendeleo ya CCM yanahitaji ushiriki wa kila mwanachama.

Mwipopo ameyasema hayo alipokuwa Mgeni Rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Iringa, ambapo amewahimiza wanawake kuendelea kuwa mstari wa mbele katika shughuli za kisiasa na kushiriki kikamilifu katika uongozi wa chama.

Amesema hakuna mwanachama anayepaswa kujiona hana nafasi katika ujenzi wa chama kwa sababu ya jinsia, kiwango cha elimu au uwezo wa kiuchumi, bali kila mmoja anapaswa kutumia uwezo alionao kwa ajili ya kuimarisha chama.

Kwa mujibu wa Mwipopo, ujenzi wa CCM unahitaji matumizi ya akili, maarifa, uzoefu na nguvu za kila mwanachama, akisisitiza kuwa ushiriki wa wanawake ni sehemu muhimu katika kuimarisha misingi ya uongozi na mshikamano ndani ya chama.

Ameongeza kuwa wanawake wanapaswa kujiamini na kutumia nafasi zinazopatikana ndani ya chama kwa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi, badala ya kubaki watazamaji katika shughuli za kisiasa.

Katika hatua nyingine, Mwipopo ametoa Shilingi milioni 4 kwa UWT Mkoa wa Iringa, ikiwa ni mchango wa kusaidia kulipia sehemu ya madeni yanayohusiana na viwanja vinavyomilikiwa na Umoja huo.

Akizungumza kuhusu mchango huo, Mwipopo amesema lengo ni kusaidia UWT Mkoa wa Iringa kupunguza mzigo wa madeni ya viwanja na kuwezesha Umoja huo kuendelea kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi.

Mchango huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono shughuli na maendeleo ya UWT Mkoa wa Iringa, huku Mwipopo akisisitiza umuhimu wa ushirikiano na mshikamano katika kuimarisha taasisi na shughuli za chama.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!