Latest Posts

AFANDE SELE ADAI KUPIGWA STOP TAMASHA LA MIAKA30 YA BONGO FLEVA, “OKTOBA 29” YAMPONZA

Mwanamuziki na mfalme wa mashairi nchini Tanzania, Selemani Msindi maarufu kama Afande Sele amedai kuwekwa kando na kuzuiwa kuendelea kutumbuiza kwenye tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva kutokana na hatua yake ya kuzungumzia na kuwakumbuka watu waliotangulia mbele za haki wakati wa matukio ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Katika tamasha hilo la Miaka 30 ya Bongo Fleva lililofanyika tarehe 7 Novemba 2026 mkoani Mbeya, Afande Sele alipanda jukwaani na kuimba akiwasihi wananchi kuwaombea na kuwakumbuka waliotangulia mbele za haki, akisisitiza kuwa matukio ya Oktoba 29 hayasauliki.  Hata hivyo, amedai waandaaji wa tamasha hilo wameelekezwa asiruhusiwe kuendelea kuwepo kwenye maonesho yanayofuata.

Akizungumza na Jambo TV, Afande Sele amedai kuwa alitakiwa kuueleza umma kwa kusema kuwa ana dharura au yuko ‘bize’ ili kuficha sababu halisi ya kuachwa kwake. Hata hivyo, amekataa katakata mpango huo akisisitiza kuwa muziki ndiyo kazi yake kuu inayomlisha na kuwa hawezi kuwahadaa wananchi

Afande Sele amebainisha kuwa kuongelea kwake matukio ya Oktoba 29 hakukuwa na nia ya kumtuhumu yeyote bali kulilenga kuiondoa taswira iliyokuwepo kuwa tamasha hilo lilikuwa la ‘machawa’ pamoja na kuitetea serikali ambayo nayo yenyewe imekiri kuwepo kwa matukio hayo na kuunda tume za uchunguzi.

“Niliongea ili kuhakikisha kwamba watu hawachukulii kama ni ‘show’ ya machawa. Naitetea show pia, lakini pia natetea nchi… Mimi sijasema kama nani kaua, sijasema hivyo… hata mimi nasubiri uchunguzi na tume zinaundwa kutafuta ukweli”, ameeleza Afande Sele.

Tamasha lijalo la Miaka 30 ya Bongo Fleva litafanyika wilayani Kahama mkoani Shinyanga tarehe 27 Novemba 2026 ambapo katika mabango ya matangazo ya orodha ya wasanii watakaotumbuiza picha ya Afande Sele haijaonekana. Hata hivyo, akizungumza na Jambo TV kwa njia ya simu, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki na mmoja wa waratibu wa tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva, Hamisi Taletale (Babu Tale), amesema kutokuwepo kwa Afande Sele kwenye orodha hiyo hakuhusiana na mambo aliyoyazungumza jukwaani katika tamasha lililopita, bali unatokana na utaratibu wa kawaida wa kubadilisha na kuwapunguza wasanii kulingana na mahitaji, idadi kubwa ya wasanii na gharama.

Ameeleza kuwa orodha ya wasanii imekuwa ikibadilishwa kutoka mkoa mmoja hadi mwingine ili kutoa fursa kwa wasanii wengi zaidi kushiriki kwenye tamasha hilo. Ametolea mfano wa wasanii wengine wakubwa ambao pia hawakuwepo kwenye maonyesho ya mikoa mingine kama vile Chege, Temba, Keisha, na Dully Sykes ambaye hakutumbuiza maonesho ya Arusha wala Zanzibar.

“Wanaenda wakipungua pungua. Mbona hujamuona Chege na Temba?… yaani watu ni wengi halafu usafiri ni ndege… Kwahiyo tunapangua pangua tu vile, yaani unamuona anakosa hapa anakuja hapa”, ameeleza Babutale.

Pia amebainisha kuwa kwenye tamasha la Kahama wameingizwa wasanii wengine wapya ambao hawakuwepo kwenye maonesho yaliyopita, wakiwemo Saida Karoli na Best Nasso. Ameeleza kuwa msimamizi wa tamasha hilo, Madee, amekuwa akiratibu ratiba hiyo ili kuhakikisha kila msanii anapata nafasi ya kushiriki katika vituo mbalimbali.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!