Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imeiomba Serikali kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa barabara ya Mbulu–Hydom hadi Singida pamoja na barabara inayounganisha wilaya hiyo na Hanang kwa kiwango cha lami, hatua inayolenga kukuza uchumi na kurahisisha usafirishaji wa mazao ya biashara kwenda kwenye masoko.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Mbwana Kambangwa, amesema kukamilika kwa barabara hizo kutachochea ukuaji wa uchumi kutokana na kuongeza mwingiliano wa wananchi na kurahisisha shughuli mbalimbali za kijamii na kibiashara.
Kambangwa amemtaka Mbunge wa Mbulu Vijijini, Dkt. Emanuel Nuwas, kulipa suala la barabara hiyo kipaumbele na kufuatilia mara kwa mara Wizara ya Ujenzi ili kuhakikisha fedha za kuendeleza mradi huo zinapatikana kwa wakati. Amesisitiza kuwa miundombinu ya usafirishaji ni muhimu katika kufikia malengo ya kukuza uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mbunge Dkt. Emmanuel Nuwas ameitaka halmashauri kupitia wataalamu wake kuweka mkakati wa kutambua na kuendeleza mazao maalumu ya biashara yatakayoweza kuitangaza Mbulu ndani na nje ya nchi. Mbulu inatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa uzalishaji wa mazao ya kilimo yakiwemo karoti, vitunguu swaumu na vitunguu maji, hivyo kuimarika kwa barabara kutarahisisha kuyafikisha sokoni.
Aidha, halmashauri hiyo imeeleza kuwa pamoja na mahitaji ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa kufikia zaidi ya asilimia 30 katika robo ya kwanza ya mwaka, hatua inayodhihirisha juhudi za kuongeza mapato kwa ajili ya maendeleo ya wilaya hiyo.
