Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limewakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 15 kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watu sita na kujeruhi wengine watano, katika tukio linalodaiwa kuchochewa na wafugaji waliokuwa wakijaribu kuwaokoa ng’ombe wao waliokuwa wamekamatwa na askari wa hifadhi ya Wanyamapori (TAWA) ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawagala, wilayani Sikonge mkoani Tabora.
Akitoa taarifa hiyo Novemba 10,2026, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora, ACP. Twaha Lulengelule, amesema tukio hilo lilitokea usiku wa manane Septemba 18, 2026, kufuatia operesheni iliyokuwa ikiendeshwa na askari wa TAWA kwa kushirikiana na askari wa Shirika la ADAP, askari wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Ipole, walinzi wa vijiji (VGS) pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge.
Kamanda Lulengelule amewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi wanapokumbana na changamoto au migogoro, akisisitiza umuhimu wa kutumia vyombo vya dola kutatua matatizo, huku akibainisha kuwa operesheni ya kuwatafuta na kuwakamata watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo ikiendelea.