Watu 21 wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi la abiria la kampuni ya Maokoto Bus Services na lori la mizigo katika eneo la Masumbo, kwenye barabara kuu ya Iringa–Mbeya.
Kwa mujibu wa taarifa za awali iliyotolewa na Afisa habari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, waliofariki ni wanaume 10, wanawake tisa na watoto wawili.
Inadaiwa kuwa ajali hiyo imesababishwa na hitilafu katika mfumo wa breki wa basi hilo, hali iliyomfanya dereva kushindwa kulidhibiti na kusababisha kugongana na lori hilo.
Mashuhuda wanasema basi hilo lilikuwa likitoka Kijiji cha Wasa, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, kuelekea Iringa Mjini wakati ajali hiyo ilipotokea.
Taarifa zaidi kuhusu hali za majeruhi na hatua zinazochukuliwa na mamlaka husika zinatarajiwa kutolewa kadri uchunguzi na taarifa rasmi zitakavyokamilika.
Jambo TV inaendelea kufuatilia tukio hilo na itawaletea taarifa zaidi kadri zitakavyopatikana.
