Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa imetenga zaidi ya ekari 500, kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), unaolenga kuwawezesha vijana na wanawake kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo.
Akizindua zoezi la ugawaji wa mashamba katika Kijiji cha Lusinga, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Atupele Mwakibete, amesema jumla ya vijana na wanawake 54 wamejitokeza kunufaika na mradi huo, ambapo kila mmoja atapatiwa ekari tatu za ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Mwakibete amesema mradi huo unalenga kuwajengea vijana na wanawake uwezo wa kufanya kilimo biashara chenye tija na kuachana na kilimo cha mazoea kilichokuwa kikilenga zaidi uzalishaji wa chakula kwa matumizi ya nyumbani.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Afisa Kilimo wa Wilaya ya Kilolo, Michael Mwaisondola, amesema halmashauri hiyo imekuwa ya 19 kutekeleza mradi wa BBT, huku Serikali Kuu ikiwezesha gharama za usafishaji wa ekari 300 ili kuyaandaa mashamba kwa ajili ya uzalishaji.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa BBT kutoka Wizara ya Kilimo, Zainabu Sheuya, amesema mradi huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa chakula na malighafi za viwanda kupitia ushiriki wa vijana na wanawake katika shughuli za uzalishaji mali.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Rashid Nzelemela, amesema mashamba hayo yatatumika zaidi kwa kilimo cha viazi na njegere, mazao ambayo yanatarajiwa kuongeza uzalishaji na kuchangia kukuza uchumi wa wananchi na halmashauri kwa ujumla.
Baadhi ya wanufaika wa mradi huo wamesema fursa hiyo itawapatia nafasi ya kujiajiri kupitia kilimo, kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia zao, huku wakitarajia kunufaika na shughuli za uzalishaji mali.
Mradi wa BBT ni sehemu ya juhudi za kukuza ajira na fursa za kiuchumi kwa vijana na wanawake nchini kupitia sekta ya kilimo, kwa kuwahamasisha kushiriki katika kilimo biashara na kuongeza uzalishaji wa mazao kwa maendeleo ya taifa.