Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Iringa, imekabidhi vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 37 kwa Klabu ya Kodi ya Shule ya Sekondari Tosamaganga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha elimu ya kodi mashuleni na kujenga kizazi chenye uelewa, uwajibikaji na utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na kompyuta 20, printa moja, mashine moja ya fotokopi, fulana 270 pamoja na vitabu na machapisho mbalimbali ya elimu ya kodi, msaada unalenga kuwawezesha wanafunzi kutumia teknolojia katika kujifunza, kufanya tafiti na kupata taarifa sahihi kuhusu masuala ya kodi na mchango wake katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Oktoba 30, 2026, Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Maigloria Saria, alisema msaada huo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na TRA wakati wa maadhimisho ya miaka 100 ya Shule ya Sekondari Tosamaganga huku akiwataka wanafunzi kutumia fursa hiyo kuimarisha shughuli za klabu na kuwa mabalozi wa elimu ya kodi katika familia na jamii zao, kwa kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari, kudai na kutoa risiti.
Saria alisisitiza kuwa kulipa kodi ni uzalendo na wajibu wa kila mwananchi, akieleza kuwa mapato ya kodi yanachangia kugharamia huduma muhimu za kijamii, zikiwemo elimu, afya na ujenzi wa miundombinu.

Kwa upande wake, Meneja wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TRA ambaye pia ni msimamizi wa Klabu za Kodi nchini, Hudson Kamoga, amesema msaada huo ni sehemu ya dhamira ya TRA ya kuimarisha klabu za kodi katika shule mbalimbali Nchini kwa lengo la kujenga kizazi kitakacholipa kodi kwa hiari, si kwa sababu ya kufuatiliwa, bali kwa kutambua kuwa ni wajibu wa kisheria na sehemu ya uzalendo.
Aidha Mkuu wa Shule ya Sekondari Tosamaganga, Laurent Manga, amesema Klabu ya Kodi ilianzishwa mwaka 2025 na kwa sasa ina wanachama 270 wanaopatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari na mchango wake katika maendeleo ya taifa huku akiishukuru TRA Mkoa wa Iringa kwa msaada huo, akieleza kuwa vifaa hivyo vitaongeza ari ya wanafunzi kushiriki katika shughuli za klabu na kuboresha upatikanaji wa maarifa.

Naye mwakilishi wa uongozi wa shule, Joshua Msafiri, alisema vifaa hivyo vitasaidia kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji, kurahisisha tafiti na kuchochea azma ya shule ya kuwa taasisi inayozingatia matumizi ya teknolojia.
Makabidhiano hayo ni sehemu ya juhudi endelevu za TRA za kuimarisha elimu ya kodi mashuleni kupitia klabu za kodi, kwa lengo la kujenga jamii yenye uelewa na uwajibikaji, inayolipa kodi kwa hiari na kutambua kuwa kodi ni msingi muhimu wa utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo ya taifa.
