Wauzaji wa nyama, wachinjaji na wamiliki wa mabucha katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wamehimizwa kupima afya zao kila baada ya miezi sita na kuzingatia kanuni za usafi mahali pa kazi ili kulinda afya zao na za walaji.
Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha maafisa mifugo, wachinjaji, wauzaji wa nyama na wamiliki wa mabucha tarehee 29/10/2026 Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Ndugu Chacha Manyinyi Mahiti, amesema baadhi ya wauzaji wa nyama hawazingatii ipasavyo kanuni za afya na usafi.
Ndugu Chacha amesema wauzaji wa nyama wanapaswa kupima afya kila baada ya miezi 6 kwa kujaza fomu maalum, kudumisha usafi wa mwili na mazingira ya kazi, pamoja na kuvaa sare maalumu wakati wa kuhudumia wateja ili kuhakikisha nyama inayouzwa ni salama kwa walaji.

Aidha, amewasisitiza wauzaji wa nyama kuepuka matumizi ya vyombo vya plastiki kuweka chakula hasa chenye joto ili kuepuka baadhi ya kemikali zilizo kwenye vyombo vya plastiki ambazo ni chanzo cha magonjwa kama saratani na mengineyo.
Sambamba na hilo, wamiliki wa mabucha wamehimizwa kusajili biashara zao na kuhakikisha wanakuwa na leseni halali za biashara kwa kufuata taratibu za Halmashauri, ili kuwezesha shughuli za uuzaji wa nyama kufanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.
Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga za kuimarisha usimamizi wa shughuli za uchinjaji na uuzaji wa nyama, kuongeza uelewa wa wadau kuhusu afya na usafi, na kuhakikisha wananchi wanapata nyama salama kwa matumizi ya binadamu.
