Serikali mkoani Geita, kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imewataka wadau mbalimbali kuimarisha juhudi za kupambana na rushwa kwa kubaini maeneo yenye viashiria vya vitendo hivyo, kujifunza kutokana na uzoefu na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha uadilifu, uwazi na uwajibikaji katika taasisi na jamii.
…
Akizungumza katika warsha ya mapambano dhidi ya rushwa ambayo imefanyika mapema leo iliyowakutanisha wadau mbalimbali wilayani Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, amesema ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi zinazopambana na rushwa ni muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka na uwajibikaji unaimarishwa katika jamii.
Komba amesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kukataa vitendo hivyo na kuwa mabalozi wa kuhamasisha maadili mema katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa GGML, Duan Campbell, amesema mgodi huo unatambua Suala la rushwa na vitendo vya ufisadi ni vibaya, na kwamba jambo la msingi ni kuchukua hatua zaidi kwa kuelewa maeneo yenye hatari ya kutokea kwa vitendo vya rushwa
Naye Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, Alex Mpemba, amepongeza ushirikiano unaotolewa na GGML, akieleza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata haki na fursa sawa bila kulazimika kutoa au kutegemea rushwa.
Warsha hiyo imekuwa sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa, huku wadau wakihimizwa kuendeleza elimu ya maadili, uwazi na uwajibikaji ili kujenga jamii inayokataa vitendo vya rushwa na inayozingatia haki na usawa.
