Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametoa wito kwa viongozi wa dini na jumuiya za kiraia nchini kuchagua njia ya maridhiano, kufuata sheria na kulinda amani ya taifa, akionya kuwa machafuko na vurugu huumiza wananchi wasio na hatia na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Katambi ameyasema hayo leo, Oktoba 28, 2026, alipokuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya usajili wa jumuiya za kiraia nchini Tanzania.
Akirejea matukio yaliyotokea huko nyuma, Katambi ameeleza kuwa nchi iliingia katika madhila na vurugu zilizosababisha kupoteza maisha, majeraha, na uharibifu wa mali za Serikali na za watu binafsi kutokana na baadhi ya watu kuamini katika vurugu badala ya maridhiano na kufuata katiba na sheria.
“Nchi yetu iliingia katika madhila ya changamoto zilizojitokeza na vurugu mbalimbali ambazo zilipelekea kupatikana kwa changamoto aidha watu kupoteza maisha ama kujeruhika ama uharibifu wa mali za serikali na za watu binafsi. Lakini hii yote ilitokana na baadhi yetu kuchagua kuamini katika vita, machafuko na vurugu kuliko maridhiano. Kuamini katika njia ya kutafuta maslahi fulani au madaraka kwa njia isiyokuwa ya kikatiba au ya kisheria… Waheshimiwa viongozi wa dini, viongozi wa jumuiya, haya yote ni sisi Watanzania kuyatafakari. Hivi kweli tunapenda vita? Hivi kweli tunapenda machafuko? Na je tuko tayari na tumejiuliza nani atabaki salama?”, amehoji Katambi.
Ameongeza kuwa pindi sheria na haki zisipofuatwa, makundi yaliyo hatarini kama vile wazee, wanawake, na watoto ndio wanaoteseka zaidi kwasababu hawawezi kukimbia pindi machafuko yanapotokea.
Katambi amebainisha kuwa Rais yuko tayari wakati wote kufungua milango na kusikiliza kero au changamoto za makundi yote katika jamii wakiwemo viongozi wa dini, wa kisiasa, na wananchi wa kawaida kama vile machinga, bodaboda, na mama lishe ili kupata suluhu kwa njia ya amani na maridhiano
“Taifa letu hatujafika huko bado tunayo nafasi ya kusahihisha na kuangalia pale tulipojikwaa kuliko kuangalia pale tulipoangukia ili tusahihishe haya yote. Na mheshimiwa rais ametoa wito mara nyingi na mara kadhaa kama kuna jambo lolote ikulu iko wazi wakati wote ametoa fursa si kwa viongozi wa dini si kwa viongozi wa kisiasa si kwa viongozi wa makundi mbalimbali… Rais wetu yuko tayari kufungua milango na kusikiliza na kwenda kutatua changamoto kwa pamoja”, ameeleza.
Ametoa rai kutoka Serikali na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa viongozi wa jamii na dini kushirikiana na Serikali kulinda amani iliyoijenga nchi kwa miaka mingi, ili Watanzania waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na biashara katika mazingira ya usalama.
“Tukilibomoa taifa letu tukaruhusu wachache waweze kuchochea vurugu na machafuko ambayo yatapelekea kupoteza amani. Pengine tunaweza tusirudi katika taifa lenye amani na usalama… Niwaombe sana tumsaidie mheshimiwa Rais katika uongozi wa nchi. Tulisaidie taifa letu katika kukuwa katika uchumi… Watanzania wanatamani kuona kuna amani. Watanzania wanatamani kuona kuna maendeleo”, ameeleza.