Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawashikilia askari 13, wakiwemo askari watatu wa Shirifisho la Hifadhi za Taifa (TANAPA), askari sita wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), na askari mgambo wanne, kwa tuhuma za kuhusika na vifo vya watu wane katika Kijiji cha Kanyamika, kilichoko wilayani Muleba.
Ka mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, aliyoitoa jana Jumapili, Oktoba 18, 2026, tukio hilo la kusikitisha lilitokea tarehe 17 Oktoba 2026, majira ya saa 4:00 asubuhi, wakati kikosi hicho kilipokuwa katika doria ya kikazi ndani ya Hifadhi ya Misitu ya Ruiga.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa vurugu ziliibuka baada ya askari hao kuwazuia watu waliokuwa wakisafirisha mkaa kwa kutumia pikipiki zipatazo kumi, ambapo inadaiwa kuwa watuhumiwa waligoma kukamatwa na kujaribu kuwanyang’anya silaha ya kivita ya aina ya AK-47 askari waliokuwepo eneo la tukio.
Kufuatia mapambano hayo, shambulio lililofuata lilisababisha vifo vya watu watatu papo hapo, ambao ni Osward Yuster (38), Pius Charles (40), na Charles Michael (35), huku mtu wa nne, Edgar Elias Lukangula (44), akipoteza maisha tarehe 18 Oktoba 2026 akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera. Katika tukio hilo la ghasia, gari moja la Serikali mali ya TFS aina ya Toyota Landcruiser liliharibiwa vibaya.
Hadi kufikia sasa, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata pikipiki 10, magunia 22 ya mkaa, mapanga matano, pamoja na silaha na risasi zilizotumiwa katika tukio hilo. Sambamba na uchunguzi unaoendelea, polisi limetoa wito mkubwa kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi ama kupambana na vyombo vya ulinzi wakati wa utekelezaji wa sheria.