Latest Posts

NAESA YATAKIWA KUSHIRIKIANA NA WATAALAMU KUINUA KILIMO KILIMANJARO

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, ameitaka Taasisi ya Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani (NAESA) kushirikiana kwa karibu na maafisa kilimo wa mkoa huo ili kuboresha huduma za ugani na kuongeza tija katika sekta za kilimo na ufugaji.

Babu ametoa wito huo Oktoba 29, 2026, alipokutana na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo waliotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuitambulisha NAESA, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha usimamizi na ufanisi wa huduma za ugani nchini.

Amesema ushirikiano kati ya NAESA na wataalamu wa kilimo ni muhimu katika kuhakikisha wakulima na wafugaji wanapata elimu, mafunzo na ushauri wa kitaalamu utakaowawezesha kutumia mbinu bora za uzalishaji. Ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza tija katika shughuli za kilimo na ufugaji, kukuza uchumi wa wananchi na kuchochea maendeleo ya sekta hizo.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa taasisi hiyo, Mkurugenzi wa Mafunzo wa NAESA, Bw. Felix Mrisho, amesema miongoni mwa majukumu ya taasisi hiyo ni kuratibu na kusimamia huduma za ugani katika sekta ya kilimo, pamoja na kuanzisha na kusimamia miundombinu ya teknolojia za kilimo.

Amefafanua kuwa katika ngazi ya taifa, NAESA itashirikiana na Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau wengine wa sekta ya kilimo katika kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini shughuli za ugani.

Ushirikiano huo unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za ugani na kuongeza ufanisi wake, ili wakulima na wafugaji wapate utaalamu na mbinu bora zitakazosaidia kuongeza uzalishaji, kuboresha tija na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo katika maendeleo ya wananchi na uchumi wa taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!