Latest Posts

TANZANIA YACHAGULIWA KUWA M/KITI KAMATI YA USIMAMIZI ENDELEVU WA BONDE LA ZIWA TANGANYIKA

Tanzania imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kikanda ya Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika, hatua inayoiweka katika nafasi ya kuongoza juhudi za kikanda za kukabiliana na changamoto za kimazingira, ongezeko la kina cha maji, kupungua kwa akiba ya samaki, na matukio ya hali mbaya ya hewa katika ziwa hilo.

Uteuzi huo umefanyika leo, Oktoba 30, 2026, mkoani Dar es Salaam wakati wa kikao cha 14 cha Mkutano wa Mawaziri wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), kinachozikutanisha nchi wanachama za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Tanzania na Zambia. Tanzania inachukua uenyekiti huo ikitambua kuwa takribani theluthi mbili ya bonde la Ziwa Tanganyika ipo ndani ya mipaka yake, jambo linaloipa nafasi ya kipekee katika kuongoza ulinzi na usimamizi wa rasilimali zake.

Akiwasilisha mtazamo wa kitaalamu wa mamlaka hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa LTA, Dkt. Emma Liwenga, alitaja changamoto kuu mbili zinazohitaji kipaumpe cha haraka kuwa ni pamoja na ongezeko la kina cha maji na kupungua kwa kiasi cha kutia wasiwasi cha akiba ya samaki, akisisitiza ulazima wa kuchukua hatua za haraka za kinidhamu na kiutafiti kulinda mustakabali wa ziwa hilo.

Akifungua kikao hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Hamad Masauni amezitaka nchi wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA) kuhakikisha kuwa juhudi za uhifadhi wa ziwa hilo zinaenda sambamba na kukuza fursa za uwekezaji rafiki kwa mazingira, ili kuchangia ajira na kipato cha jamii bila kuhatarisha mfumo wa ikolojia.

“Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa uhifadhi wa ziwa unaenda sambamba na maendeleo ya kiuchumi… na fursa za uwekezaji rafiki kwa mazingira ili kuchangia ajira na kuongeza kipato cha jamii bila kuhatarisha uwezo wa ziwa wa kuendelea kutoa huduma muhimu za kiikolojia”, ameeleza Masauni.

Waziri Masauni amebainisha kuwa Ziwa Tanganyika ni miongoni mwa rasilimali zenye thamani kubwa Afrika na duniani, na kwamba uamuzi wa nchi moja ndani ya bonde hilo una athari moja kwa moja kwa nchi jirani, akisisitiza kuwa Ziwa Tanganyika linahitaji utashi thabiti wa kisiasa na uwajibikaji wa pamoja kati ya nchi zote zinazolizunguka ili kulinda rasilimali hizo kwa uendelevu.

“Ziwa Tanganyika linahitaji utashi wa nchi husika katika kuhakikisha kwamba ulinzi wa rasilimali zetu kwa pamoja linakuwa ni endelevu na jukumu letu sote. Hivyo basi niwahimize nchi wanachama tuendelee kushughulikia ama kutathmini maamuzi ya pamoja”, ameeleza.

Aidha, ameeleza kuwa katika mtazamo wa kidiplomasia ya kikanda, ziwa hilo ni mfano wa jinsi rasilimali za pamoja zinavyoweza kujenga ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo endelevu, huku akisisitiza kuwa Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika una nafasi muhimu ya kuimarisha uratibu kati ya mataifa hayo manne.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Kijani na Mazingira wa Jamhuri ya Zambia, Dkt. Douty Chibamba Akiwasilisha msimamo wa Jamhuri ya Zambia, mwakilishi wa nchi hiyo amethibitisha kuwa Zambia itaendelea kushirikiana bega kwa bega na serikali za Burundi, DRC, na Tanzania katika kulinda na kusimamia rasilimali za Ziwa Tanganyika.

Naye Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Jean-Pierre Tshimanga Buana amebainisha kuwa washiriki wa mkutano huo ndio watekelezaji wakuu wanaotegemewa katika kuleta matokeo na uendelevu wa ziwa hilo. Hivyo, ametoa wito ulitolewa kwa LTA kuwakusanya wadau wote wakubwa wanaozunguka ziwa hilo ili kuunganisha nguvu katika kutatua changamoto za kiikolojia zinazokabili ziwa hilo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!