Serikali mkoani Geita imeanza mazungumzo na mamlaka mbalimbali, ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Geita, kutafuta maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya mpira wa kikapu katikati ya miji, hatua inayolenga kukuza mchezo huo na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Hatua hiyo imekuja huku baadhi ya wadau wakionesha nia ya kusaidia ujenzi wa miundombinu ya mchezo huo ili kuimarisha maendeleo ya mpira wa kikapu mkoani humo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa wadau na wachezaji wa mpira wa kikapu Jana tarehe 30 Oktoba 2026 ,iliyofanyika katika viwanja vya mchezo huo vilivyopo Jimbo la Geita Mjini, Afisa Michezo Mkoa wa Geita, Rogers Bahati, amesema serikali inaendelea kuonesha mwitikio katika kuunga mkono maendeleo ya mchezo huo.

Bahati amesema kuna kila sababu ya kuishukuru serikali kwa jitihada zake za kusaidia michezo, akieleza kuwa uwepo wa miundombinu bora utaongeza fursa kwa vijana kuendeleza vipaji vyao na kujipatia ajira kupitia michezo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Geita, Rashid Shaban, amesema chama hicho kimeanza mkakati wa kuwafundisha watoto wadogo mchezo huo ili kuwajengea uwezo tangu wakiwa na umri mdogo.
Amesema hatua hiyo inalenga kukuza vipaji vya watoto, kuandaa wachezaji wa baadaye na kuhakikisha mpira wa kikapu unaendelea kupata maendeleo mkoani Geita.