Serikali ya Tanzania imelipa Dola za Marekani milioni 32 (sawa na takriban Shilingi bilioni 74 za Kitanzania) ili kuipatia nchi uhalali wa kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mwaka 2027.
Hatua hiyo imebainishwa leo, Septemba 24, 2026, na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya michezo na usimamizi wa nembo za taifa.
Waziri Makonda ameeleza kuwa mbali na kitita hicho cha Dola milioni 32 cha uenyeji, Serikali pia ipo katika mazungumzo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ili kulipa Dola za Marekani milioni 12 (takriban Shilingi bilioni 30) kwa ajili ya kupata haki za matangazo ya televisheni (broadcast rights) ya mashindano hayo.
Amefafanua kuwa fedha hizo si za ujenzi wa viwanja au miundombinu ya barabara, bali ni uwekezaji wa kimkakati wa kuitangaza Tanzania duniani, kukuza utalii, na kutengeneza fursa za ajira kwa vijana
“Tumelipa sisi taifa kuwa wenyeji wa AFCON milioni 32… Sawa na bilioni takriban 74. Hii ni pesa ya kuwa tu mwenyeji. Lakini pia tunazungumza na CAF tunatakiwa tulipe dola milioni 12 ya kupata haki za matangazo. Hizi fedha sio za kujenga uwanja, sio za kununua maji, sio za kufanya kujenga barabara. Kama nchi tumelipa ili tupate uhalali wa kuhosti haya mashindano. Namba mbili tupate uhalali wa kuitangaza taifa letu kupitia mashindano ili watakaokuja waje wakiona Tanzania ni sehemu sahihi ya kuwekeza, vijana wengi wapate ajira”, ameeleza Makonda.
Waziri Makonda amesisitiza kuwa kutokana na Serikali kuwekeza mabilioni hayo ya fedha, jezi ya Timu ya Taifa (Taifa Stars) ni vazi kuu linalotambulisha nchi na nembo inayopaswa kuongezewa thamani kubwa ya kimasoko badala ya kuchukuliwa kwa wepesi au kutangazwa bila uratibu rasmi.