Latest Posts

NANAUKA AWATAKA WANAFUNZI KUJIANDAA KWA USHINDANI WA SOKO LA AJIRA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Dk. Joel Arthur Nanauka, amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati kujenga maarifa na ujuzi mpana ili kukabiliana na ushindani wa maisha, kutumia fursa zilizopo na kutokata tamaa wanapokumbana na changamoto.

Akizungumza na wanafunzi mkoani Iringa kupitia programu ya Campus Connect, amesema vijana hawapaswi kujikita katika taaluma wanazosomea pekee, bali wanapaswa kupanua uelewa wao katika masuala mbalimbali yanayowazunguka ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na mazingira ya maisha.

Amesema kuwa mwanachuo anapaswa kuwa na maarifa na ujuzi mpana utakaomwezesha kutumia fursa zilizopo, kutatua changamoto na kujitofautisha katika soko la ajira.

Akitumia dhana ya Survival of the Fittest, Dk. Nanauka amewahimiza vijana kujituma, kujiamini na kujiandaa kukabiliana na ushindani mkubwa uliopo katika maisha badala ya kukata tamaa wanapokutana na vikwazo.

Kupitia programu hiyo, wanafunzi wamepata fursa ya kuuliza maswali na kuwasilisha changamoto zinazohusu ajira, ujasiriamali na fursa za maendeleo, huku wakijadiliana moja kwa moja na kiongozi huyo.

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki wamepongeza programu ya Campus Connect wakieleza kuwa imewapa nafasi ya kutoa maoni yao, kueleza changamoto zinazowakabili na kupata maarifa yatakayowasaidia katika kupanga mustakabali wao.

Aidha, wanafunzi hao wameahidi kuyafanyia kazi maarifa na mafunzo waliyoyapata kupitia majadiliano hayo ili yaweze kuwasaidia katika safari yao ya kujiletea maendeleo.

Programu ya Campus Connect inalenga kuimarisha mawasiliano kati ya viongozi na wanafunzi wa vyuo, kuwapa vijana nafasi ya kutoa mawazo yao na kushiriki katika mijadala inayohusu maendeleo yao pamoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!