Latest Posts

NGAJILO ATOA JEZI KUSAPOTI MICHEZO KWA VIJANA IRINGA MJINI

 

Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Fabian Ngajilo, ametoa jezi kwa timu mbalimbali za mpira wa miguu za wanaume katika jimbo hilo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha na kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana.

Ngajilo amekabidhi jezi kwa timu hizo kwa lengo la kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika michezo, huku akisisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya, nidhamu na kukuza vipaji miongoni mwa vijana.

 

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Ngajilo amesema anaendelea kuunga mkono jitihada za vijana katika michezo na kwamba msaada huo ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za kukuza michezo ndani ya Jimbo la Iringa Mjini na Mkoa wa Iringa kwa ujumla.

Mbali na jezi za mpira wa miguu kwa wanaume, Mbunge huyo pia ametoa mipira kwa ajili ya mchezo wa rede kwa wanawake, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika michezo na kuwapa nafasi ya kuendeleza vipaji vyao.

Ngajilo amesema michezo ina nafasi kubwa katika kuwaweka vijana pamoja, kujenga ushirikiano na kuwaepusha na vitendo visivyofaa, hivyo wadau mbalimbali wanapaswa kuendelea kushirikiana katika kuibua na kukuza vipaji vya vijana.

Kwa upande wao, wawakilishi wa timu zilizopokea vifaa hivyo wameishukuru hatua hiyo, wakisema msaada huo utawapa hamasa zaidi wachezaji kuendelea kushiriki katika michezo na kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

Wamesema pamoja na changamoto za vifaa na miundombinu ya michezo, jitihada kama hizo zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha michezo katika jimbo hilo na kuwapa vijana fursa ya kutumia vipaji vyao kujenga maisha yao.

Hatua ya Ngajilo inatajwa kuwa sehemu ya mwendelezo wa shughuli za kuunga mkono michezo na vijana katika Jimbo la Iringa Mjini, huku akitoa wito kwa vijana kutumia fursa hizo kwa kujituma, kuzingatia nidhamu na kuendelea kuiwakilisha vyema Iringa katika medani ya michezo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!