Latest Posts

MWANACHAMA WA SIMBA AHOJI THAMANI YA KLABU, AIBUA HOJA KUHUSU UWEKEZAJI WA SH BILIONI 20

Mwanachama wa Simba Sports Club, Abuu Changawa, mwenye kadi namba 22924, ameeleza wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa uongozi wa klabu hiyo, akitaka maslahi ya wanachama na mustakabali wa timu kupewa kipaumbele katika maamuzi yanayohusu uwekezaji na usimamizi wa klabu.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Iringa, Changawa amesema mgogoro unaoendelea kati ya Bodi ya Wakurugenzi na Kamati ya Utendaji unapaswa kuchunguzwa kwa kina, kwa kuzingatia Katiba ya Simba pamoja na nafasi ya wanachama katika kulinda mali na thamani ya klabu hiyo.

Kuhusu suala la uwekezaji, Changawa amepinga kufanyika kwa maamuzi ya kimuundo na umiliki wa klabu bila kuwepo kwa tathmini huru na ya kina itakayobainisha thamani halisi ya Simba.

Amedai kuwa thamani ya klabu hiyo inaweza kufikia Sh bilioni 250, akisisitiza kuwa kabla ya kujadili kiwango cha uwekezaji au asilimia ya hisa zitakazotolewa, ni muhimu kufanyika kwa tathmini inayozingatia mali za klabu, shughuli zake za kibiashara na uwezo wake wa kuzalisha mapato.

Kwa mujibu wa Changawa, Simba si klabu ya mpira wa miguu pekee, bali ni taasisi yenye wanachama na mashabiki wengi ndani na nje ya Tanzania, ambao anaamini ni sehemu muhimu ya mtaji na nguvu ya kiuchumi ya klabu hiyo.

Kutokana na hoja hiyo, amehoji mantiki ya kujadili uwekezaji wa Sh bilioni 20 bila kuwepo kwa taarifa za wazi zinazoeleza namna kiwango hicho kilivyopatikana, vigezo vilivyotumika kukikadiria na manufaa yatakayopatikana kwa klabu na wanachama wake.

Changawa amesisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wanachama katika maamuzi makubwa yanayohusu mustakabali wa Simba, akieleza kuwa tathmini sahihi ya thamani ya klabu ni hatua muhimu kabla ya kuchukua maamuzi yoyote kuhusu uwekezaji na umiliki wake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!